Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ameeleza kuwa baadhi ya wanasiasa mpaka kuisha kipindi hiki cha Kampeni, wataokota makopo kwa kukosa uelekeo wa siasa.
Ameyasema hayo tarehe 19 Septemba, 2020 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Kyerwa, Kagera."Wanaohama kutoka CCM wakidhani wananguvu, wakitoka wanageuka kama vichaa, wafuatilieni wote waliohama CCM, hakuna mwanaCCM maarufu kuliko CCM,"
Aidha Dkt. Bashiru amefafanua kuwa "Ukiona we maarufu ujue umeazimwa umaarufu huo na CCM , siku Chama kikikutupa ama ukikitupa umaarufu unakoma hapo hapo. Wapo watakaookota makopo ninawahakikishia."
"Kuna watu wapo miguu juu kama mende, tena miguu juu kwa raundi moja ya kampeni wakati zipo sita, wamejileta wenyewe, wajanja kama mzee Mrema na Cheyo wakasema hapa tunamuunga mkono Magufuli, waliobaki wote tusilaumiane, tutatumia nguvu zote za CCM bila kujali udhaifu wao, tutatumia uwezo wetu wote bila kujali udhaifu wao, tutawashinda, hadharani kwa kishindo.." Katibu Mkuu ameeleza
Aidha, Katibu Mkuu ameeleza namna Chama kilivyojipanga kuhakikisha kinaboresha maslahi ya wakulima na kukata mirija ya wanyonyaji katika biashara ya mazao ikiwemo zao la Kahawa.
"Tunataka kufanya utafiti badala ya kutegemea zao moja la kahawa. Hatumaanishi kwamba tunaliacha, tunataka pia kujenga viwanda vya kusindika, kile kiwanda kilichokufa cha TANICA tunataka kukifufua, tunataka kuimarisha ushirika kwa kuwa na viongozi wenye uweledi, waaminifu na waadilifu."
Katibu Mkuu amefafanua pia kwa kueleza kuwa, "Tunataka muwe na sauti kuhusu bei ya kahawa yenu, lakini tunataka kukata mirija ya unyonyaji wa jasho lenu , kama mirija ipo kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya tutaikata, kama ipo kwenye polisi tutaikata, kama ipo kwa walanguzi tutaikata, kama ipo kwenye Chama tutaikata, sasa si kutumbua majipu, zamu inayokuja ni kukata mirija ya unyonyaji."
Kikao hiko, kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, wakiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Ndg. Wilbroad Mutabuzi
Kikao hiko ni mfululizo wa vikao vya ndani vinavyoendelea nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha umoja, mshikamano, nidhamu na ushirikiano, kuhakikisha ushindi mkubwa unapatikana katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020.
Imetolewa na;
Said Said Nguya
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)