MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt.
Hussein Ali Mwinyi amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha Serikali ambayo ataingoza itakuwa Serikali inayosikiliza
wasomi na wananchi wote bila kujali matabaka au makundi.
"Ahadi yangu kwenu vijana endapo mambo yatakuwa mazuri nitahakikisha Serikali nitakayokwenda kuiongoza inakuwa Serikali sikivu inayosikiliza wasomi na wananchi kwa ujumla,"amesema Dkt. Mwinyi.
Hayo ameyasema leo Septemba 1, 2020 huko Tunguu Kusini Unguja wakati akihutubia vijana kwenye mhahalo wa vijana wa CCM uliomdaliwa na Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu ambapo lengo la mdahalo huo ni kujadili mambo mbalimbali kwa mustakabali wa CCM.
Dkt.Mwinyi amesema kwamba, endapo harakati zitakamilika na kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha kuwa Serikali atakayoiunda inawasikiliza wote kuanzia wasomi na wananchi kwa ujumla.
"Hauwezi kuwa na Serikali ambayo haitawasikiliza watu. Mimi nataka niwaahidi kwamba Serikali ambayo ntakwenda kuitengeneza itawasikiliza wasomi na wananchi wangu,"amesema Dkt.Mwinyi.
Dkt.Mwinyi pia amewatoa hofu vijana wa CCM kwamba Serikali inayokuja itahakiksha inakwenda kuendeleza yale yote yaliyofanywa na awamu iliyopita katika kutatua changamoto zinazokabili watu wenye ulemavu.
Hata hivyo Dkt.Mwinyi ametoa wosia kwa vijana hao kuhakikisha wanakwenda kwenye kampeni na Uchaguzi Mkuu huku wakihubiri amani na utulivu.
"Tunakwenda katika uchaguzi mkuu, hivyo wosia wangu kwenu hakikisheni mnahubiri amani...amani na tunaitunza hiyo amani iliyopo nchini, twendeni tukafanye kampeni za kistarabu,"amesema Dkt. Mwinyi.
Tags
Siasa