Dkt.Hussein Mwinyi:Wajasiramali, wavuvi, wakulima baada ya Oktoba 28 mtafurahia kazi zenu, tupeni kura zote

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais atawawezesha wajasiriamali kupata fursa za mikopo,mafunzo na masoko ili wajikwamue kiuchumi.

Dkt.Mwinyi amesema suala la ujasiriamali limepewa kipaumbele katika sera za CCM, hivyo kupitia mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi watatoa mikopo yenye masharti nafuu ili iwasaidie wajasiriamali hao.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na makundi mbalimbali ya wajasiriamali katika mwendelezo wa ziara yake ya kukutana na wananchi huko katika Kijiji cha Michenzani Wilaya ya Mkoani Pemba.

Dkt.Mwinyi amesema, wajasiriamali wakiwezeshwa watapata fursa ya kutengeneza bidhaa zenye viwango zinazokubalika katika masoko ya kitaifa na kimataifa.

Amesema, katika Serikali ijayo sekta ya ujasiriamali itapewa uzito wa kipekee, kwani inawawezesha wanawake na vijana kujiajiri wenyewe.

“Wanawake na vijana msiwe na hofu ujasiriamali ni sekta muhimu sana katika maendeleo ya nchi yetu hasa kwa wakati huu wa kuelekea katika uchumi mpya kwa maslahi ya wananchi wote,"amesema

Pia amesema ataendeleza mazuri yaliyofanywa na Serikali inayomaliza muda wake sambamba na kubuni vyanzo vipya vya kiuchumi vitakavyoongeza pato la taifa na kuiwezesha serikali kutoa ajira nyingi kwa wananchi. 

Amesema, atatekeleza kwa vitendo vipaumbele vyake ambavyo ni kuimarisha huduma za kijamii zikiwemo kuboresha huduma za afya,elimu na upatikani wa huduma za maji safi na salama kwa wakati.

Amesema kuwa, ataimarisha sekta za miundombinu zikiwemo ujenzi na utanuzi wa barabara,kuimarisha miundombinu ya umeme na ujenzi wa bandari mpya zitakazotoa ajira kwa wingi.

Akizungumzia sekta ya uvuvi amesema, atahakikisha wanapata vifaa vya kisasa vya uvuvi vitakavyowasaidia kuondokana na uvuvi wa zamani usiokuwa na tija.

“Nafahamu wavuvi na wakulima wa mwani mnakabiliwa na changamoto nyingi hasa ukosefu wa nyenzo za kisasa za uvuvi, nakuahidini nikipata kuwa Rais matatizo yayayowakabili nitayatatua,”amesema Dkt.Mwinyi.

Awali Katibu wa Jumuiya ya Wavuvi katika Kijiji cha Mwambe Mpene Wilaya Mkoani, Kheri Sheha Ali amesema wanakabiliwa na changamoto ya kutumia vifaa duni vya uvuvi hivyo wanaomba kupatiwa vifaa vya kisasa.

“Vyombo vyetu ni vya zamani kuna wakati baadhi ya wenzetu wanapoteza maisha kutokana na vifaa hivi, hivyo tunaomba serikali itupatie boti za kisasa,”amesema.

Mgombea huyo wa Urais wa Zanzibar, Dkt.Mwinyi aliwaombea kura wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi za urais hadi madiwani ili washinde katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news