DOTO BITEKO AANZA SAFARI YA KURUDI BUNGENI KWA KUTAJA MAFANIKIO YA MIAKA MITANO

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Bukombe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Doto Biteko amefungua mkutano wa kampeni ya kuomba kura kwa kipindi cha awamu ya pili kwa kubainisha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika jimbo hilo kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, anaripoti ROBERT KALOKOLA kutoka GEITA.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa ufunguzi wa kampeni za uchunguzi mkuu wa 2020 katika uwanja wa Uyovu wilayani Bukombe,Doto amesema mwaka 2015 jimbo hilo lilikuwa na zahanati mbili ,lakini hadi sasa wanajenga zahanati kila kijiji.
Mgombea Ubunge Jimbo la Bukombe Doto Biteko akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Uyovu wilayani Bukombe.PICHA NA ROBERT KALOKOLA/www.diramakini.co.tz.

Ameongeza kuwa, jimbo hilo lilikuwa na kituo cha Afya Uyovu kikiwa na hali mbaya lakini katika kipindi hiki cha miaka mitano kimepata milioni 500 ambazo zimetumika kukiboresha na kinatoa huduma nzuri na kuwa na uwezo wa kufanya hata upasuaji.

CCM mkoa wa Geita wamezindua kampeni za uchaguzi mkuu kwa Rais,wabunge na madiwani katika uwanja wa Uyovu wilayani Bukombe kwa ngazi ya mkoa na baada ya hapo majimbo mengine yatakuwa na kazi ya kuendelea na mikutano yake Kama kawaida.

Biteko amesema kuwa, jimbo hilo kabla ya mwaka 2015 halikuwa na barabara ya lami lakini kwa kipindi cha miaka mitano Serikali imejenga barabara ya lami kutoka Uyovu kuelekea Geita.

Aidha,amesema kuwa, wilaya hiyo ilikuwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji,lakini zimetumika zaidi ya bilioni 5 kujenga miradi ya maji.

Kwenye sekta ya elimu,Doto Biteko amesema kuwa kulikuwa na msongamano wa wanafunzi madarasani,lakini hadi sasa wanaendelea kujenga shule mpya tatu kwa ajili ya kumaliza tatizo hilo.

Ameongeza kuwa,ameamua kugombea kwa kipindi cha pili ili kuendelea kutatua changamoto mbalimbali katika jimbo hilo.

Kuhusu umeme amesema, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) umefikisha umeme katika vijiji 70 ambavyo amesema alilazimika vitongoji 20 kuvipa hadhi ya vijiji ili kuweza kupata umeme kwa haraka.

Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita kimezindua kampeni zake katika jimbo hilo la Bukombe ambapo Mwenyekiti wa Mkoa wa Geita, Alhaj Said Kalidushi amesema,wana uhakika watashinda kwa asilimia 100.

Kalidushi amesema kuwa, CCM imetekeleza ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 kwa ufanisi mkubwa,hivyo anaamini wananchi watachagua chama hicho.

Kalidushi akiwatambulisha wagombea ubunge wa majimbo mbalimbali katika mkoa huo waliofika ambao ni Constantine Kanyasu mgombea wa Jimbo la Geita Mjini , Nicodemus Maganga Mgombea Jimbo la Mbogwe na Dkt.Medard Kalemani mgombea wa Jimbo la Chato.

Doto Biteko ambaye hadi sasa ni Waziri wa Madini aligombea kwa mara ya kwanza katika Jimbo la Bukombe mwaka 2015 na kufanikiwa kushinda.

Doto Biteko alichukua jimbo hilo kutoka mikononi mwa Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Profesa Kulikoyela Kahigi aliyeshinda jimbo hilo mwaka 2010.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,Doto Biteko alishinda Jimbo hilo kwa kupata kura 47,147 dhidi ya Profesa Kahigi aliyepata kura 29,929 na Dickson Bagamba wa ACT alipata kura 1,673.

Katika uchaguzi wa Mwaka huu,Doto Biteko anachuana na mgombea wa Chadema Renatus Nzemo ambaye alikuwa Katibu wa Kanda ya Serengeti.



Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news