HALOPESA, UMOJA SWITCH WAZINDUA HUDUMA YA KUTOA FEDHA KWA NJIA YA ATM



Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Halopesa, Magesa Wandwi (kulia) na Afisa Mkurugenzi Mkuu wa UmojaSwitch,Danford Mbilinyi wakikabidhiana mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Halopesa na UmojaSwitch, ambapo wateja wa Halopesa nchini wataweza sasa kutoa pesa katika ATM za umoja zilizopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini. NA MPIGA PICHA WETU.

KUTOKANA na kasi ya ukuaji wa teknolojia na uchumi, Halopesa imeendelea kutanua wigo wa kutoa huduma zake za kifedha nchini ikizingatia pia mkakati wa kitaifa wa ujumuishwaji wa wananchi katika matumizi ya mifumo rasmi ya kifedha chini, anaripoti MWANDISHI WETU.

Ikiwa ni mwendelezo wa kuwafikia na kuwapa wateja wa Halopesa huduma bora kwa urahisi na uhakika, Halotel kupitia huduma yake ya HaloPesa imeingia ubia na Kampuni ya UmojaSwitch kutoa huduma kwa wateja wa HaloPesa ya kutoa fedha kupitia ATM za Umoja zilizoko kote nchini.

Afisa bidhaa na masoko wa Halopesa,Roxana Kardio akitoa maelekezo jinsi ya kutoa pesa kwenye ATM za Umoja katika mojawapo ya ATM za umoja jijini Dar es Salaam.NA MPIGAPICHA WETU.

Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hii katika ofisi za Makao Makuu ya Halotel, Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Halopesa, Magesa Wandwi amesema kuwa, ni hamasa na lengo lao ni kuhakikisha kuwa, "tunaendelea kutumia miundombinu ya teknolojia na fursa zote zilizopo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta hii ya huduma za kifedha na kuwapa wateja wetu huduma bora na za uhakika na ni furaha yetu leo kushirikiana na UmojaSwitch kuzindua rasmi huduma hii ambayo itawawezesha wateja wa HaloPesa kutoa fedha kwa urahisi na uhakika zaidi kupitia ATM za Umoja zaidi ya 250 zilizopo maeneo mbalimbali kote nchini.

"Tunapenda kuwasisitizia wateja wetu kuwa huduma hii haitakuwa na makato ya ziada tofauti na makato ya kawaida ya kutoa pesa kwa wakala wa kawaida, lakini pia huduma hii haitahusisha matumizi ya intaneti pale ambapo mteja atakuwa anatoa fedha kwenye ATM za Umoja,"amefafanua Wandwi.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Halopesa,Magesa Wandwi (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa huduma ya kutoa pesa kwenye ATM za Umoja katika makao makuu ya ofisi za Halotel jijini Dar es Salaam,amesema huduma hiyo itawawezesha wateja wote wa Halopesa kutoa pesa kupitia ATM zote za Umoja. Kushoto ni Afisa Mkurugenzi Mkuu wa UmojaSwitch,Danford Mbilinyi. NA MPIGAPICHA WETU.

"Kwa huduma hii pamoja na mawakala wetu zaidi ya 50,000 waliosambaa nchini kote kwa pamoja tutaendelea kuwahudumia wateja wetu wa Halopesa zaidi ya 2,000,000 waliopo mijini na vijijini.


Afisa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya UmojaSwitch,Danford Mbilinyi (kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Halopesa,Magesa Wandwi, kwa pamoja wakisaini Mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Halopesa na UmojaSwitch. Akishuhudia kulia ni Afisa Mawasiliano Halotel, Hindu Kanyamala na kushoto ni Adellah Kaihula Afisa Masoko wa UmojaSwitch. PICHA NA MPIGAPICHA WETU.

"Mteja wa Halopesa atapitia hatua za kawaida kutoa pesa kwa kupiga *150*88# kisha kuchagua ‘2’, (Kutoa Pesa ), Kisha chagua tena “2” (UmojaATM), ataendelea na kuweka kiasi na namba yake ya siri ya Halopesa, baada ya hapo atapata ujumbe wenye namba ya siri ya uthibitisho ambayo ataitumia kutoa fedha katika ATM za Umoja,"amebainisha Mkuu huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa UmojaSwitch, Danford Mbilinyi amesema, ushirikiano na Halopesa utaongeza upatikani wa huduma za kifedha kirahisi nchini, "kupitia ATM zetu zaidi ya 250 zilizoenea nchi nzima," amesema na kuongeza kwamba wateja wa HaloPesa wana fursa nyingine ya uhakika sasa ya kupata fedha muda wowote mahali popote nchini.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news