Hati Fungani mkombozi wa jamii iliyothubutu kuwekeza, ndiyo njia mwafaka kufanikisha malengo yako

UWEKEZAJI wa pamoja unaweza kuwa kitu kipya kwa Watanzania wengi, japo Kampuni ya Uwekezaji (UTT AMIS) imekuwepo tangu mwaka 2005 ikihamasisha uwekezaji wa aina hiyo.

Katika nchi nyingine duniani, uwekezaji wa aina hiyo umekuwepo muda mrefu. Kwa mfano, India Unit Trust of India imekuwepo tangu mwaka 1963.

India Unit Trust of India ni kampuni ya Serikali, ilikaa sokoni kwa miaka 24 bila mshindani ndipo zikaanza kuanzishwa kampuni binafsi za Uwekezaji wa Pamoja.

Hadi sasa, kuna kampuni zaidi ya 2,500 za uwekezaji wa pamoja. Nchini Marekani kuna kampuni zaidi ya 10,000 zote zikijaribu kuwavuta wawekezaji ili washiriki kwenye uwekezaji huo wenye mafanikio makubwaa duniani.

Mifuko ya uwekezaji wa pamoja iko aina mbalimbali ili kukidhi malengo ya wawekezaji. Wapo wawekezaji ambao wanataka kipato cha mara kwa mara.

Wengine wanataka kukuza mtaji, elimu kwa watoto, uwekezaji na bima mfano ya maisha au ulemevu wa kudumu, kipato ndani ya muda mfupi na malipo kwa haraka zaidi.

Mifuko hiyo ipo inayowekeza kwenye hisa, hati fungani, kwenye benki lakini iko mingine haiwekezi kwenye hisa, inawekeza kwenye hati fungani tu na kwenye bidhaa za benki mfano Mfuko wa Hati Fungani wa UTT AMIS.

Mtu mwenye nia ya kuwekeza kwenye Hati Fungani anaweza kushawishiwa kwenda kununua hati fungani sokoni badala kununua kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja unaosimamiwa na UTT AMIS.

Mwekezaji anaweza kuwa sahihi, lakini anaweza kukosa faida zifuatazo. Mosi, Mfuko wa Hati Fungani wa UT AMIS ni njia mpya ya uwekezaji katika uwekezaji wa pamoja ambayo awali haikuwepo nchini.

Siku za nyuma mtu binafsi au kampuni mbalimbali zilikuwa zikienda moja kwa moja kununua hati fungani za muda mfupi au mrefu.

Hivi sasa inawezekana watu, makundi mbalimbali, kampuni na Serikali hukusanya fedha zao pamoja chini ya Meneja UTT AMIS ambaye ataziwekeza fedha hizo kwa niaba yao na kila mtu kupata faida au hasara kama itakuwepo japo.

Katika hali ya kawaida, huo ni uwekezaji salama kwa kampuni iliyopo chini ya Serikali, lakini uwezo wa kampuni binafsi kulipa ni mdogo sana.

Ni vigumu mtu binafsi kuwa na fedha za kutosha ili kununua hati fungani ya kampuni binafsi ila kwenye Uwekezaji wa Pamoja, kwa kuwa fungu la pesa ni kubwa, Meneja UTT AMIS anaweza kuwekeza asilimia nane kwa kampuni binafsi, asilimia 92 hati fungani za Serikali za miaka tofauti.

Kupitia Mfuko wa hati Fungani, si lazima uwe tajiri ili kuwekeza katika hati fungani, unaweza kuanzia sh.5,000 ambazo zitatosha kuanza kununua hati fungani baada ya kipindi cha zuio kuisha.

Hii ina maana kuwa, hata yule mwenye kipato kidogo ana nafasi ya kuwekeza. Kwa kufanya bei kuwa ndogo kuna vuta mtaji mkubwa wa kuwekeza.

Mtaji ukiwa mkubwa maana yake nguvu ya majadiliano inakuwa kubwa na gharama za uendeshaji zinakuwa ndogo, hii ina maana kuwa wigo wa faida unaongezeka.

Wenye mtaji mdogo wanafaidi na punguzo la gharama linalopatikana kupitia uwekezaji wa pamoja.

Ujuzi tofauti kwenye hisa mfano kuwekeza kwenye hati fungani kuna hitaji uchunguzi bobezi zaidi mfano kujua uwezo na tabia ya anayeuza hati fungani.

Hata kama ni Serikali hali ya kiuchumi ikoje, tegemeo la baadae likoje mfano thamani ya fedha, mfumuko wa bei, mambo mengine muhimu kama riba.

Hati Fungani daima ni tulivu ikitoa fursa ya kujikinga na kujijenga.

Kwanini uwekeze katika Hati Fungani? Katika Dunia ya sasa, hati fungani inawakilisha uwekezaji usio na mawimbi makubwa. Wakati hisa zinatawala vichwa vya habari, hati fungani inawalinda na mdororo wa uchumi.

Hati fungani huwa ni kimbilio lao kwani mara nyingi bei ya hati fungani inakwenda kinyume na riba zake.

Ni ukweli usiopingika kuna wakati hisa zinalipa sana, lakini ni rahisi kutabiri mwenendo wa hati fungani ukilinganisha na ule wa hisa.

Uzuri wa hati fungani ni kwenye uhusiano wake na uchumi, wakati nchi inataka kuendeleza miradi zaidi inahitaji pesa, pia wakati uchumi unadorora pesa zinahitajika ili kuuweka sawa, hati fungani kila wakati imekuwa kati ya jawabu la uhakika.

Mara nyingi uwekezaji unategemea malengo, muda na uvumilivu wa hali hatarishi ambatanishi.

Umri unaenda, mahitaji ya kipato cha mara kwa mara yanakuwa makubwa hivyo Mfuko wa Hati Fungani ndiyo suluhisho ukisonga mbele na hausimami.

KUINUA KIPATO

Kwa kawaida, hati fungani za Serikali zinalipa faida kwa uhakika sana, lakini faida yake mara nyingi ni ndogo ukilinganisha na hati fungani za kampuni.

Ili kupata kipato kizuri unashauriwa kuchanganya hati fungani za kampuni binafsi na Serikali.

Kuna kampuni binafsi zingine hazina historia kama ziko kwenye misingi mizuri ya kuweza. Kimsingi unapaswa kuchukua tahadhari kubwa.

Mambo yakiwa mazuri faida inakuwa kubwa ila yakienda mrama huzuni inaweza kutawala. Kampuni zisizoaminika zinaweka riba nzuri ili kuvuta wawekezaji.

Hati fungani za muda mrefu zina unafuu wa kodi. Hii ni nzuri kwa mwekezaji kwani inamuhakikishia kipato zaidi.

Tukumbuke kuwa, ukinunua hati fungani ina maana umekopesha fedha zako kwa Serikali kama hati fungani hiyo ni ya Serikali pia kwa kampuni kama hati fungani hiyo ni ya kampuni kwa muda maalum na riba iliyokubaliwa.

Tukumbuke pia mwekezaji anaweza kununua hati fungani moja kwa moja, hii inakuwa rahisi kama mtaji ni mkubwa, pia awe anaweza kusubiri kupata gawio kila miezi sita, awe na subira ya kupata mkopo.

Hati fungani zipo za miaka tofauti. Pia tukumbuke kuwa, mwekezaji anaweza kuuza hati fungani yake kama atahitaji pesa zake na atauza akipata mnunuzi.

Kwenye Mfuko wa Hati Fungani (Bond Fund) unaweza kuwekeza kiasi kidogo cha mtaji na kupata gawio mara kwa mara, si lazima usubiri miezi sita, utauza hati fungani yako muda wowote bila shida.

Ukinunua hati funagani moja kwa moja unapata faida kama mlivyokubaliana yani kama kila miezi sita asilima saba itakuwa hivyo na asilimia iliyokubaliwa baada ya muda kuisha itakuwa hivyo pia.

Lakini ukinunua kupitia uwekezaji wa pamoja itategemea thamani ya kipande, hivyo mwekezaji atafaidi thamani ya kipande iko juu, ikiwa ndogo faida inaweza kupungua.

Badilika, chukuwa hatua, wengi tunatamani kuwa matajiri, wengi tunatamani fedha zao ziwe nyingi zaidi, lakini woga ndiyo shida yetu.

Waswahili wanasema woga wako ndiyo umaskini wako, Watanzania wengi hawapendi kuthubutu, wanaogopa.

Kumbuka hakuna maajabu duniani, lazima tuwekeze ili kuongeza kipato chetu. Wengi wetu tuna pesa zimekaa tu nyumbani au benki bila kufahamu fedha hizo tungezipa thamani zaidi kwa kuziwekeza sehemu salama kama kwenye Mfuko wa Hati Fungani.

Wale waoga wa kuwekeza hupenda kupitia kwenye mifuko ambayo ni salama sana. Unaweza kupata faida, lakini itakuwa ya wastani.

Ili upate faida kubwa ni muhimu kuwekeza sehemu zenye hali hatarishi kidogo. Mfano mifuko inayochanganya hati fungani na hisa. Hisa ni chachu ya faida pia ni chachu ya hasara. Mara nyingi Hati Fungani zitakupa faida ambayo mara chache sana yaweza kuwa zaidi ya asilimia 15 hadi 16.

Mara nyingi maamuzi ya wapi uwekeze yanaendana na malengo, umri, muda, faida tarajiwa. Kwa mfano, mtu anayekaribia kustaafu ataridhika na faida ya wastani.

Hatapenda kuwekeza sehemu ambayo ni hatarishi, kwani pengine hana nguvu ya kuhangaika tena ili kutafuta. Hicho alicho nacho kinaweza kuwa turufu yake ya mwisho.

Kwa vijana wanaweza kuthubutu, kwani wana muda wa kuanguka na kusimama kwa nguvu zaidi. Wana muda wa kujifunza kutokana na makossa yao.

Siku hizi kuna usemi unaosema, jifunze kutokana na makossa ya wenzio, usisubiri mpaka uanguke ndio ujifunze kutokana na makosa yako.

Malengo yanaweza kukufanya uwe na msimamo wa woga mfano mtu anayeweka fedha ili kununua nyumba, ada ya shule ni tofauti na mtu anayewekeza ili kwenda kutalii.

Nyumba na ada ya shule ni lazima, lakini kutalii si lazima. Pesa ya nyumba na ada ya shule unaweza kuiweka katika hali ambayo si hatarishi sana.

Pesa ya utalii unaweza kuiwekeza katika mradi ambao una viashiria vya hatari zaidi ambavyo vikienda sawa vinakupa faida nzuri zaidi.

Kwa mwekezaji mwenye malengo ya muda mrefu anawezakuanza kuwekeza sehemu ambayo inaweza kumpa faida sana au sehemu ambayo faida tarajiwa ni kubwa sana huku dhoruba zake zikiwa juu kama zitatokea.

Kadri muda na lengo lako linavyokaribia, unaweza kuhamisha uwekezaji katika maeneo yenye hatari za uwekezaji kidogo na faida za wastani. Ili uweze kupata ufanisi ushauri ni muhimu, unaweza kutembelea Ofisi za UTT AMIS.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news