Haya ndiyo haukuweza kuyasikia haraka kutoka kwa Mgombea Urais Dkt.John Magufuli kutoka Kigoma hadi Tabora leo

Akiwa njiani kutoka Kigoma kuelekea  mkoani Tabora,Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. John Magufuli amelazimika kufanya mikutano midogo midogo kila anapokuta na maelfu kwa maelfu ya wananchi wanaomsubiri kumsikiliza na kutoa ahadi .
Moja ya ahadi ambazo ametoa akiwa njiani kuelekea Tabora ni ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Uvinza hadi Maragalasi yenye urefu wa kilometa 151 na kwamba fedha kwa ajili ya ujenzi huo zipo.

"Tumetengeneza huko kote pamebakia hapa, hatuwezi kupaacha, hii barabara fedha zipo, sizungumzi kwa sababu ya kampeni, msema kweli mpenzi wa Mungu.Fedha zipo ndio maana nimepita hapa sio kwa helkopta, bali kwa gari nione changamoto ya barabara hii,"amesema .

Amesisitiza kuwa, barabara hiyo inatarajiwa kuanza kujengwa kuanzia Oktoba, mwaka huu na kwamba watatangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami.

Pia amezungumzia ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 10 ambayo itajengwa katikati ya Mji wa Uvinza, ambapo ametumia nafasi hiyo kumpigia simu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Serikali za Mikoa na Tawala za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo ili apeleke fedha shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo.

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Mheshimiwa Dkt.John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Kaliua mkoani Tabora katika mkutano wa kampeni za CCM leo tarehe 20 Septemba 2020.



Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Isawima Kaliua mkoani Tabora katika muendelezo wa kampeni za CCM leo tarehe 20 Septemba 2020.

Ameagiza fedha hizo ziwe zimefika kuanzia wiki ijayo. Pia Dkt.Magufuli amezungumzia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe kutoka Nsibwa hadi Kaya kilomita 237 pamoja na madaraja.

"Tutajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Changu hadi Kazilambwa, tumeipangia katika bajeti hii,"alisema.

Kuhusu nishati, Dkt. Magufuli amesema, Uvinza imechelewa sana, kwani katika vijiji 61 ni vijiji 17 tu ndivyo vimefikiwa na umeme, huku akifafanua katika umeme Uvinza haijafanya vizuri.

"Naomba mnipe kura tukafanye ya ukweli kwa nchi nzima kwa mwaka 2015 vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa 2018, leo hii tuna vijiji 9,700, vimebaki vijiji 2,500 vikiwemo na vya hapa Uvinza,"amesema Dkt.Magufuli.

Ameongeza kuwa, atawabana vizuri watu wake akiwemo Waziri wa Nishati ambaye anaamini anasikia changamoto hizo na kumtaka asikilize na kuanza kuzitekeleza, kwani bado ni Waziri wa Nishati.

Pia amemtaka Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, akamueleze Waziri wa Nishati Dkt. Merdard Kalemani kwamba suala la umeme Uvinza hajafurahishwa nalo, kwani kati ya vijiji 61 vilivyowekwa umeme ni 17 tu.
 

Magufuli amesema ni lazima suala hilo alibebe mwenyewe, kwani Uvinza kuna kiwanda cha Chumvi ambacho kinatakiwa kutangazwa ili kuuza chumvi hadi nchi za Burundi, DRC na Uganda kwani ukifika utasaidia vijana kupata ajira.
 
Akizungumzia kukatika kwa umeme mara kwa mara,Magufuli amesema ni changamoto ya muda mrefu kwa Uvinza na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, lakini kupitia mradi mkubwa wa umeme katika bwawa la Julius Nyerere ambalo litazalisha umeme megwati 2,115 zitatumika katika gridi ya Taifa na hivyo kuunganisha Uvinza  na Mkoa wa Kigoma na Kagera.

"Naomba mniamini ndugu zangu katika hili, ambapo kwa mwaka itatumika sh.bilioni 2.18 na hadi kukamilika kwa mradi huo jumla ya sh. bilioni 26.16 ili kutatua tatizo hilo,"amesema.

Sekta ya afya, amesema ujenzi wa miundombinu ya afya imejengwa maeneo mbalimbali ya Uvinza, ikiwemo pamoja na kuongeza bajeti ya dawa ambayo imesaidia kuboresha huduma za afya, maabara, nyumba za watumishi.

Aidha, kwa upande wa elimu, alisema nako kuna jitihada ambazo zimefanyika ambapo sh.bilioni 5.04 zimetumika kwa ajili ya maendeleo ya Wilaya ya Uvinza.

Amesema, wamepeleka sh.bilioni 7.63 kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo ambayo imetoa fursa ya elimu kwa watoto wa Uvinza.

Akizungumzia kuhusu maji, Magufuli amesema miradi yenye thamani ya sh.bilioni 11.06 imetekelezwa katika Wilaya ya Uvinza na mingine inaendelea kutekelezwa.

Mgombea huyo akiwa Kazuramimba,ameahidi kuchangia sh.milioni 10 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kazuramimba mkoani Kigoma baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.

Ujenzi wa kituo hicho ulianza kwa nguvu za wananchi. Dkt.Magufuli alisema lazima kituo hicho kimalizike ujenzi wake, hivyo atakapochaguliwa na kushinda urais atatoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kukamilisha kituo hicho.

"Najua nitashinda urais, hivyo katika kipindi cha miezi mitatu tutakuwa tumekamilisha ujenzi. Hiki ni kipindi cha kampeni, hivyo nikitoa hizi hela ambazo nataka kuchangia watasema natoa rushwa, ndiyo maana nasema nitatoa baada uchaguzi kwisha,"amesema.

"Wananchi wa Kazuramimba umeonesha mfano mzuri sana kwa kuamua kuanza ujenzi kwa nguvu zenu na wanasema mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe.Nami niwaahidi wananchi wa hapa nitachangia ujenzi wa kituo hiki cha afya,"amesema.

Amesema atapeleka dawa na vifaa tiba pamoja na watalaam ili kituo kianze kutoa huduma za matibabu ili kiwe kinatoa na huduma za upasuaji."Tunataka hiki kituo cha afya kiwe kinafanya na operesheni," alisema.

Dkt. Magufuli amesema kutokana na umuhimu wa kituo hicho, Waziri wa Afya ambaye atamteua kazi yake ya kwanza itakuwa ni kushughulikia kituo hicho ili kianze kazi ya kutoa huduma kwa wananchi hao.

Wakati huo huo Dkt. Magufuli ameendelea kuzungumzia mkakati ya kuboresha miundombinu ya barabara kilomita 51 kwa kiwango cha lami kutoka Kazuramimba hadi Uvinza ambapo amesema, fedha hizo tayari zipo, hivyo wananchi watatoka hapo hadi Dar es Salaam bila kukanyaga changarawe.

Dkt. Magufuli akiwa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora ameahidi kufufua reli ya kutoka Kaliua - Mpanda ili kuwezesha wananchi wafanye biashara vizuri.

Rais Dkt Magufuli kwa upande wa maji amesema upo mpango wa kuyavuta kutoka Tabora kupitia Urambo hadi Kaliua ili kumaliza changamoto ya uhaba wa maji wilayani hapo.

Pia amesema, atafanyia kazi kero ya barabara ya lami Kaliua Mjini, mahakama ya wilaya, ofisi ya Mamlaka ya Mapato (TRA), Magereza ya wilaya, uhaba wa watumishi wa afya na barabara za vijijini ambazo nyingi huwa hazipitiki hasa nyakati za mvua, hivyo kuwasababishia wananchi usumbufu ikiwemo ujenzi wa barabara inayounganisha Kaliua hadi Katavi.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 423 anasema itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi katika kuharakisha shughuli za maendeleo huku akisisitiza kuwa mahitaji ya wakulima wa pamba pia yatapewa kipaumbele zaidi.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news