CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Musoma Mjini kimezindua kampeni zake leo katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara ambapo kimewaomba wananchi wa jimbo hilo kukichagua katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kuanzia Madiwani, Mbunge na Rais ili kiweze kuwatumikia wananchi kwa kuwaletea maendeleo hususan kuimarisha huduma za kijamii na mfumo bora wa maisha,anaripoti AMOS LUFUNGILO kutoka MARA.
Uzinduzi wa kampeni hizo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti,Ester Matiko, Mgombea Ubunge Jimbo la Bunda Mjini Ester Bulaya na Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime Vijijini John Heche ambao walinadi sera za chama hicho na kumuombea Kura Mgombea wa Jimbo la Musoma Mjini Julius Mwita.
Akizungumza na wananchi pamoja na wanachama wa Chadema Mgombea Ubunge Kupitia (Chadema) Jimbo la Musoma Mjini Julius Mwita, amewaomba wamchague katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu awezekwenda bungeni kuzungumzia Maendeleo ya Jimbo la Musoma Mjini ikiwemo kushughulikia upatikanaji wa huduma bora za afya ikiwemo dawa, vitanda, Vifaa tiba katika Zahanati na Hospitali Musoma mjini.
Mwita ameongeza kuwa, ataimarisha mfumo bora wa biashara kwa Wajasiriamali, sanjari na kuboresha sekta ya elimu kwa kufuta baadhi ya michango midogo midogo ikiwemo ya walinzi ambayo hutozwa katika baadhi ya shule na kuimarisha huduma ya vyoo mashuleni ili kuongeza ufaulu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti na Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime Mjini,Ester Matiko, amesema kuwa iwapo Chadema ikichaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu itahakikisha inafanya mageuzi makubwa ya kiuchumi hususan kutumia fursa zilizopo Mkoa wa Mara za madini, Ziwa Victoria na mpaka wa Sirari viweze Kukuza uchumi wa Mkoa wa Mara.
Matiko ameongeza kuwa, chama hicho kitahakikisha kinasimama kidete kwa kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa na uhakika wa huduma za kijamii ikiwemo matibabu hasa kila mtanzania kuwa na bima ya Afya sanjari na kuimarisha mfumo wa huduma za upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kuanzia zahanati mpaka hospitali za mikoa tofauti na ilivyo sasa, na hivyo akahimiza wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini kumchagua mgombea anayetokana na chama hicho pamoja na madiwani na Rais.
Naye Mgombea Ubunge Kupitia (Chadema) Jimbo la Bunda Mjini Ester Bulaya akizungumza katika mkutano huo amesema kuwa Chadema kikichaguliwa kitahakikisha kuwa kinaendelea kutetea haki za wanyonge, pamoja na kupigania haki, usawa na demokrasia Nchini huku akisisitiza wananchi kutochagua mtu kutokana na uchumi alio nao bali mwenye kuweza kutetea maslahi ya wananchi.
John Heche akimnadi Mgombea wa Jimbo la Musoma Mjini Kupitia (Chadema) Julius Mwita katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho Jimbo la Musoma Mjini leo.(Picha na Amos Lufungulo).Mgombea Ubunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, John Heche amesema wananchi wanapaswa kuchagua Chama hicho kuanzia ngazi ya udiwani hadi Rais kiweze kutengeneza mfumo bora wa maisha kwa Watanzania kwa kuondoa umaskini wa kipato kwa mwananchi mmoja mmoja.
"Tunatana haki, Uhuru na Maendeleo ya Wananchi, kutatua tatizo la ajira, wazee Wetu wamesomesha watoto kwa shida wakiuza hadi nyumba wakitegeme myoto akihitimu masomo yake ataajiriwa, lakini kwa Sasa Jambo hili halipo sisi Chadema tutafanya haya tunaomba Watanzania mtupe ridhaa ya kuongoza nchi hii tutengeneze mzunguko wa ajira," amesema.
"Mkoa wa Mara tuna fursa ya mbuga ya Serengeti na Ziwa Victoria kwa hiyo fursa hii ni muhimu Sana kukuza uchumi, tunahitaji kuwa na uwanja wa Ndege mkubwa ili watalii watue Musoma wakuze uchumi wa Mara lakini mambo haya yameshindikana, yatawezekana tu iwapo watu wa Musoma Mjini mtamchagua mgombea wa Chadema apiganie haya,"2amesema.
Aidha,viongozi hao waliondoka uwanjani kwa maandamano ya amani ambayo yaliongozwa na Mgombea ubunge Jimbo la Musoma Mjini Julius Mwita, Ester Bulaya na John Heche na wafuasi wa chama hicho kuelekea ofisi za Chadema zilizopo Nyakato ambapo shughuli zilisimama kwa muda watu wakitazama msafara huo na wenye magari pia wamesimama kwa muda.
Tags
Siasa