Hivi ndivyo basi la Golden Dragon lilivyochomwa moto kukwepa deni

JESHI la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu watatu akiwemo mmiliki wa basi la Golden Dragon kwa tuhuma za kuchoma basi hilo moto na kusingizia limewaka lenyewe kutokana na matatizo ya kiufundi katika breki huku wakilitorosha eneo la tukio.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa ameyasema hayo leo mjini hapa wakati akitoa taarifa juu ya tukio hilo.
Amesema, Agosti 27 majira ya saa nane usiku walipata taarifa katika kituo cha polisi wilayani Mvomero kuwa kuna gari linawaka moto eneo la Wami Luhindo barabara kuu ya Morogoro kwenda Dodoma wilayani Mvomero, ndipo askari polisi walifika eneo hilo na kukuta basi hilo likiwaka moto.

Kamanda amesema, baada ya askari hao pamoja na askari wa zimamoto na uokoaji kufika eneo hilo walikuta basi lenye namba T. 321  DKW, aina ya Golden Dragon mali ya kampuni ya HBS linalomilikiwa na Ahmad Hemed (25) mkazi wa Dar es Salaam, linalofanya safari zake Dar es Salaam kwenda Tabora likiwaka moto, huku dereva akidai breki za basi hilo zilikorofisha na kupelekea kuwaka moto.

“Askari polisi waliwahi kufika eneo hilo la ajali ya moto na kukuta watu watatu akiwemo mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Riziki Abraham, na kudai kuwa alikuwa akiendesha gari hilo na walikuwa wakitokea Dar es Salaam wakielekea Dodoma kuchukua wanafunzi wa chuo cha CBE kuwapeleka Tabora, walipofika eneo hilo ndipo breki za basi hilo 'zilijam' na kusababisha kuwaka moto,"amesema Kamanda huyo.

Pia amesema kwa ushirikiano wa askari wa zimamoto na polisi walifanikiwa kuuzima moto huo na kufanya uchunguzi wa awali, ndipo walipobaini basi hilo halikuwa na 'chases', injini, difu, usukani wala viti vya abiria, na kuwataka wahusika wa gari hilo kufika kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi, ndipo walipoamua kulitorosha gari hilo na kulipeleka Dar es Salaam.

Kamanda huyo amesema, baada ya kufanya ufuatiliaji walifanikiwa kulikamata gari hilo katika kituo cha mafuta cha ATN kilichopo Nanenane Manispaa ya Morogoro likiwa limeegeshwa katika lori namba T. 336 DDX  Scania R400 yenye tela namba T331 DDX likiendeshwa na dereva aitwaye Sadam Seif  kwa ajili ya kuelekea Dar es Salaam.

Amesema,watuhumiwa hao walipohojiwa kwa mara nyingine akiwemo mmiliki wa basi hilo wamesema gari hilo halikupata ajali ya moto kama ilivyoonekana na walivyozungumza awali, bali ilikuwa ni mpango wa kulichoma kwa kuwa lilikuwa linadaiwa na taasisi moja ya kifedha ambayo jina lake limehifadhiwa.

“Hivyo alipanga njama hiyo ya kulifikisha eneo hilo, kulimwagia mafuta ya 'thinner na petrol' kisha kuliwasha moto ili bima ilipe taasisi hiyo ya kifedha cha zaidi ya shilingi milioni 200 zinazodaiwa,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news