Mganga Mkuu wa Serikali,Prof.Abel Makubi amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa taasisi, vyuo vya afya, na waganga wafawidhi kuhakikisha wanawafuatilia kwa karibu wanataaluma wa afya waliopo katika mafunzo kwa vitendo , yaani watarajali (interns) ili waweze kupata umahiri, utalaamu na maadili yanayotegemewa.
Prof. Makubi ameyabainisha hayo wakati akiongea na wasajili wa Mabaraza ya Kitaaluma yaliyopo chini ya Wizara ya Afya katika ukumbi wa wizara jiji Dodoma.
Prof. Makubi amesema Serikali imeanza kupata changamoto za baadhi ya Hospitali kushindwa kuwapa mafunzo stahili wataraji hao na kujikuta wanamaliza mafunzo yao bila umahiri unaotegemewa katika kutoa huduma kwa wananachi.
""Serikali imeanza kuchunguza hizo hospitali na kama hazitasimamia vyema hawa wanataaluma walio mafunzoni, tutazifutia kibali cha kuwapokea,"amesisitiza.
Aidha, Prof. Makubi amewataka wanafunzi walio kwenye mafunzo kwa vitendo kujituma katika mafunzo yao, kuonyesha nia ya kujifunza na kuweka bidii katika mafunzo yao ya vitendo mahali walipo.
"Hawa wanataaluma wanapaswa kuonyesha tabia njema wakati wa mafunzo, kuwa watiifu, kulinda viapo vyao kuzingatia maadili ya taaluma zao na kujiheshimu katika lugha zao na hata mavazi wanayovaa mbele ya wateja wao ambao wengi ni wagonjwa na ndugu zao,"ameongeza.
Hata hivyo, Prof. Makubi ameyaagiza mabaraza hayo kuhakikisha utaratibu wa watarajali 'interns' wote kufanya mitihani baada ya mafuzo, uharakishwe ndani ya mwaka huu ili serikali iweze kupima umahiri wa wanataaluma wote wanaomaliza mafunzo kwa vitendo.
Prof. Makubi amelipongeza Baraza la Famasi kwa kuratibu mitihani kwa wafamasia wataraji na kulitaka Baraza la Madaktari nalo likamilishe utaratibu wa mitihani kwa madaktari watarajali wote ili kulinda hadhi ya taaluma ya tiba na viwango vya kutoa huduma kwa wananchi.