HOSPITALI ya Rufaa Mkoa wa Geita imeanza kutoa huduma ya tiba kwa wagonjwa mbalimbali wa nje (OPD) ikiwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa takribani 500 kwa siku ambao watapunguza msongamano kwenye hospitali nyingine za chini, anaripoti ROBERT KALOKOLA kutoka GEITA.
Mgonjwa akipata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita mapema leo baada ya kuanza kutoa huduma ya matibabu.Picha na Robert Kalokola/www.diramakini.co.tz
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt.Shaban Massawe ameieleza www.diramakini.co.tz kuwa, hospitali hiyo imeanza kutoa huduma za wagonjwa wa nje na baadhi ya huduma ni kama idara ya meno,koo, mahabara,upasuaji na huduma ya magonjwa ya wanawake na watoto.
Dkt.Massawe amesema, idadi hiyo ya wagonjwa ni kubwa hivyo itamaliza tatizo la msongamano wa wagonjwa katika hospitali nyingine za kawaida katika mkoa huo ikiwemo kwenye vituo vya afya na zahanati.
Ameongeza kuwa, watu wote wenye magonjwa mbalimbali wanaruhusiwa kufika katika hospitali hiyo kutibiwa,lakini inakuwa nzuri zaidi wenye magonjwa ambayo hayakuweza kutibika hospitali za wilaya kufika na barua za rufaa kutoka kwa daktari wa huko ili madaktari wa hospitali hiyo ya rufaa waweze kuanzia matibabu pale ambapo daktari wa hospitali za chini alipoishia kumtibu.
Amefafanua kuwa,mgonjwa anaruhusiwa kwenda kutibiwa kwa mara ya kwanza kwa kuanzia palepale hospitali ya rufaa lakini kwa kupewa barua ya rufaa kutoka hospitali za chini ni vizuri zaidi.Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita jengo la wagonjwa wa nje(OPD) ambalo limeanza kutoa huduma za tiba leo Septamba 7,2020.Picha na Robert Kalokola/www.diramakini.co.tz
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake,Ernest Nkwabi amesema kuwa huduma zote za kujifungua,kuchunguza saratani ya shingo ya kizazi na sehemu za kike ,upasuaji pamoja na uchunguzi kwa wanawake wenye matatizo ya uzazi zinatolewa katika hospitali hiyo.
Amesema kuwa, wanawake wote wenye matatizo ya uzazi wanaweza kufika katika Hospitali hiyo kwa ajili ya uchunguzi na ushauri wa kitabibu zinazo tolewa na madaktari bingwa katika hospitali hiyo.
Huduma nyingine amesema kuwa, ni kutoa elimu hasa kwa mama mjamzito na kuhudumia mwananmke anayejifungua ambaye wanakaa naye kwa muda wa saa 24 baada ya kujifungua na huduma za wagonjwa wa ndani(IPD).
Baadhi ya wananchi waliofika katika hospitali hiyo kwa siku kwanza kupata huduma ya matibabu akiwemo Esther Malimi ,Grace Mashine na Angela Agastine waneieleza www.diramakini.co.tz kuwa huduma zinazotolewa na watumishi wa hospitali hiyo ni nzuri.
Mwezi Agosti mwaka huu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia na Watoto Ummy Mwalimu,akiwa ziarani Geita aliagiza viongozi wa Mkoa wa Geita kuhakikisha Jengo la Wagonjwa wa Nje(OPD) linaanza kutoa huduma ndani ya wiki mbili.
Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Geita ilianza kujengwa mwaka 2017 chini ya Mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo ya Serikali(TBA) ambayo imejengwa eneo la Magogo Kata ya Bombambili Halmashauri ya mji wa Geita.