Baada ya mmoja wa Mahakimu nchini Somalia kuchukua hatua za kutekeleza adhabu ya moja kwa moja kuwaadhibu wanaume wawili watuhumiwa wa makosa ya ubakaji kwa watoto na wanawake mjini Mogadishu, Somalia hali hiyo inaripotiwa kurejesha nidhamu kwa kiwango kikubwa.
Mmoja wa waandishi wa habari kutoka nchini Somalia ameieleza Diramakini kuwa, kwa sasa nidhamu imeendelea kujengeka huku asilimia kubwa ya wanaume waliokuwa na tabia ya kutekeleza vitendo hivyo vya kikatili kwa wanawake wakirejesha heshima kwa wanawake.
"Nidhamu na heshima imezidi kurejea kwa wanawake, hapa Mogadishu na kule Puntiland ilikuwa kila siku lazima usikie taarifa za visa vya ubakaji, lakini kwa sasa hali imetulia.
"Ukizungumza na wanaume wengi wanaeleza namna ambavyo tukio lile (miezi kadhaa iliyopita) la mmoja wa hakimu kuripotiwa kuchukua uamuzi wa kuziondoa sehemu za siri za wale vijana wawili walioripotiwa kumdhalilisha na kumbaka binti wa miaka 10, zilikuwa habari na tukio la kushangaza kidogo, lakini kwa namna moja au nyingine nidhamu imerejea sasa,ukipita katika maeneo mengi hapa utaona namna ambavyo mdogo kwa mkubwa wanavyoanza kuheshimiana vivyo hivyo mkubwa kwa mdogo,"Mwandishi huyo ameieleza Diramakini.
Tukio hilo la hakimu kuchukua uamuzi huo ambalo picha zake zilisambaa kwa kasi mitandaoni awali, licha ya kulaaniwa na watetezi wa haki za binadamu, lakini linatajwa kusaidia kunusuru mamia ya mabinti ambao walikuwa wanatendewa uovu huo.
Juhudi za Diramakini kutaka kupata taarifa kutoka mamlaka husika nchini Somalia ili kufahamu juu ya takwimu halisi na namna walivyofanikisha kudhibiti vitendo vya ubakaji zinaendelea.
Taifa la Somalia ambalo lipo Upembe mwa Afrika limekuwa likikabiliwa na matukio mbalimbali ya kikatili kutokana na kukosekana kwa mifumo imara ya uongozi kwa miaka mingi, huku matukio mengi yakihusishwa na magaidi wa kundi la Alshabab.