IGP Sirro:Wataingia barabarani kwa sababu ipi? 40 wanashikiliwa Pemba,msituchokoze

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Saimon Sirro amesema kuwa, watu 40 wanashikiliwa na jeshi hilo kisiwani Pemba, anaripoti Mwandishi Diramakini.

"Kaskazini Pemba, nazungumzia wale wahalifu ambao waliwakata mapanga baadhi ya wakereketwa wa CCM (Chama Cha Mapinduzi), wamewajeruhi walikuwa wanatoka msikitini. Lakini watu zaidi ya 40 wamekamatwa, lakini ninachotaka kusema, wale wanajaribu...

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania (IGP),Simon Nyakoro Sirro akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo wakati akiwa mkoani humo kwa ziara ya ukaguzi Septemba 23, 2020. (Tanpol).

Ameyasema hayo Septemba 23,2020 baada ya kufanya ziara ya ukaguzi mkoani Pwani, amesema kuwa,
...wanajaribu na toka jana tumeimarisha ulinzi sana, na kikubwa zaidi nasikia wengine wanasema hawa watu wote wanaonisikiliza wataingia barabarani, niseme wale watu wote wanaokwenda kwenye ule mkutano wanaenda kusikiliza sera.

"Wala hawaendi kwa ajili ya kuandaliwa kuingia barabarani, kwa sababu watu wanaokwenda pale wote wana akili timamu na hekima zao, hawaendi pale kwa sababu ya kuhamasishwa kuingia barabarani, wanaenda pale kusikiliza sera, kwamba utawafanyia kitu gani, kwa hiyo jambo la msingi, sasa hivi kila Mtanzania anaelewa...kimsingi niwaambie Watanzania wenzangu suala la amani na utulivu ni la msingi sana,"
amesema IGP Sirro kwa sauti na video bonyeza kiambatanisho hiki https://twitter.com/tanpol/status/1308779140749942784?s=20 .

 IGP Sirro amesema kuwa, Jeshi la Polisi limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama hasa katika kipindi hiki cha kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar na kwamba yeyote atakayejihusisha na uhalifu au uvunjifu wa amani atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Wakati huo huo, Mkuu wa Jeshi La Polisi nchini Tanzania, IGP Sirro amesema Jeshi la Polisi nchini limeendelea kuimarisha usalama husasani maeneo ya bandari bubu ambazo zimekuwa zikitumika kuingiza bidhaa za magendo na wahamiaji haramu na kukwepa ushuru wa Serikali.

IGP Sirro amesema hayo wakati ziara hiyo ya ukaguzi mkoani Pwani ambapo amezitaka idara zote za Serikali zilizopo katika Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyojitokeza katika eneo hilo.

ZANZIBAR

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuwa watulivu na kuwa na imani na Jeshi la Polisi kutokana na tukio lililotokea huko kisiwani Pemba la kupigwa mapanga watu watatu wakiwa katika sehemu ya kufanyia Ibada, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo huko katika ukumbi wa mkutano Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Kiswandui Mjini Unguja.

Catherine amesema, Chama Cha Mapinduzi kinalaani vikali kitendo hicho cha kinyama ambapo kinaashiria uvunjifu wa amani.

“Nchi bado ina amani nawataka wanachama kuwa watulivu, kuondosha hofu kwani Jeshi la Polisi linafanya kazi yake na wahusika wanafuatiliwa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao,”amesema.

Ameongeza kuwa, kufanya hivyo ni kuwatia hofu wanachama wa CCM huko Pemba jambo ambalo litawaletea woga siku ya kupiga kura na wataogopa kufika vituoni na kuchagua viongozi wanaowataka.

“Kufanya hivyo ni kutaka kuwatia hofu ili muogope kwenda kupiga kura, lakini ondosheni hofu na ikifika siku jitokezeni kwa wingi kwenye vituo vya kupiga kura, kwani vyombo vya ulinzi vitaimarishwa zaidi,”amesema Catherine.

Hata hivyo amesema, CCM kipo bega na bega kwa wahanga hao na kitaendelea kuwaunga mkono, “CCM sio chama cha kulipiza kisasi, kwa mambo ambayo hayafai katika jamii, kwani chama hiki hufuata miongozo iliyopo ndani ya ilani na kinaongoza vizuri na kukubalika na jamii kuongoza dola,”amesema.

Catherine amelipongeza Jeshi la Polisi kwa juhudi zao kubwa wanazotumia katika kulinda na kudumisha amani nchini hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news