MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi ameahidi kuwa nafasi nyingi za uteuzi katika Serikali atakayoiunda ya Mapinduzi ya Zanzibar wanawake watapewa kipaumbele kwani ndio nguzo ya chama hicho.
Dkt. Hussein aliyasema hayo leo wakati akitoa salamu katika Kongamano Maalum la Wanawake lililofanyika katika ukumbi wa Amani CCM Mkoa, ambapo Mgeni Maalum katika kongamano hilo alikuwa Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na Mgeni Rasmi alikuwa Mwenyekiti wa UWT, Gaudentia Mugosi Kabaka.
Katika salamu zake hizo, Dkt.Hussein Mwinyi amesema kuwa, anauhakika mkubwa kwamba CCM itashinda kutokana na wagombea wake wa uongozi kuungwa mkono na makundi yote ndani ya chama hicho wakiwemo wanawake ambao ndio jeshi kubwa la CCM.
Amesema kuwa, wanawake wamekuwa wakifanya vizuri pale wanapopewa nafasi ya uongozi kwani wamekuwa wakionesha uadilifu wao mkubwa.
Dkt. Hussein ameeleza kuwa, katika kampeni zote za CCM wahamasishaji wakubwa ni wanawake ambao mara zote wamekuwa kitu kimoja katika kukiunga mkono na kukitetea chama chao cha CCM.
Ameongeza kuwa, umefika wakati wagombea wote wanawake wa CCM waliogombea nafasi mbali mbali zikiwemo za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kuwa kitu kimoja ili kuhakikisha chama chao kinaendelea kuongoza dola na kupata ushindi wa kishindo.
Katika salamu zake hizo, Dkt. Hussein Mwinyi ametoa wito kwa wanawake kuendelea kukitetea chama hicho na kuhakikisha kinapata ushindi na kuweza kuongoza Serikali.
Aidha, Dkt.Hussein ameeleza kuwa, kampeni kubwa za chama hicho zitafanywa majukwani lakini zaidi zitafanywa katika mikutano ya ndani.
Sambamba na hayo, Dkt.Hussein Mwinyi amesisitiza haja ya kuendelea kuitunza amani kwani bila ya amani hakuna maendeleo.
Ikulu).
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) “Umoja Wetu Wanawake Ndio Nguvu Yetu”lililofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Mkoa wa Mjini Amani jijini Zanzibar lililowashirikisha viongozi wa UWT na wagombea Ubunge na Uwakilishi Zanzibar. (Picha na
Ikulu).
Mapema mgeni Maalum wa Kongamano hilo Mama Mwanamwema Shein katika hotuba yake ameeleza kuwa, kongamano hilo maalum limeandaliwa na Umoja wa Wake wa Viongozi kwa kushirikiana na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT).
Mama Shein alitumia fursa hiyo kuwasihi wanawake pamoja na wananchi wote kuzingatia umuhimu wa kutunza amani iliyopo hivi sasa na baada ya uchaguzi.
Ameeleza kuwa, bila ya amani hakuna lolote linaloweza kufanikiwa kwani bahati mbaya ni kuwa wanawake na watoto ndio wanaoathirika sana wakati amani na usalama vinapotoweka.
“Tumuombe Mwenyezi Mungu atujaalie tuweze kushiriki katika uchaguzi Mkuu kwa amni, salama na utulivu,"amesema Mama Shein.
Mama Shein ametoa pongezi zake kwa wanawake kwa kuchagua kauli mbiu ya kongamano hilo isemayo “Umoja wetu ndio nguvu yetu”, na kueleza kuwa anakubaliana na kauli mbiu hiyo kutokana na ukweli na umuhimu wake.
Amesema kuwa, wanawake wakiwa pamoja ndio watakuwa na nguvu zaidi ya kufanya uamuzi unaofaa kwa faida yao na kusisitiza kuwa uamuzi unaofaa hivi sasa ni kuipigania CCM ili ishinde katika nafasi zote za uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Tusisahau maneno ya wazee wetu yasemayo “Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”.
Aidha, Mama Shein amesema kuwa, umoja na mshikamano ni mambo ya msingi katika kukipatia ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi na kuwataka wagombea wa nafasi mbalimbali katika chama hicho ni vyema wavunje makundi yao na waunge mkono wagombea wote waliopitishwa na CCM na kuendelea kuwa kitu kimoja.
Pamoja na hayo amesema kuwa, Mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt. Hussein Mwinyi ni mtu makini, mwenye uzoefu mkubwa katika uongozi na anaependa maendeleo.
Nae mgeni rasmi katika kongamano hilo Mwenyekiti wa UWT, Gaudentia Kabaka aliwataka wagombea wote wanawake waliogombea nafasi mbalimbali za uongozi kuwa kitu kimoja na kufahamu kuwa huo walioupata ni uteuzi si ushindi kwani wapo walioshinda kwa kura nyingi, lakini hawakuteuliwa na badala yake wameteuliwa wale wenye kura kidogo.
Ameeleza kuwa, CCM ni chama kikubwa na kueleza kuwa wanawake wanajukumu kubwa la kutafuta kura za Ubunge, Uwakilishi, Udiwani pamoja na Urais wa Jamhuri ya Muungano na Urais wa Zanzibar.
Ametumia fursa hiyo kuupongeza mchakato wa kuwapata viongozi ndani ya CCM ulivyofanyika na kuwataka wagombea ndani ya CCM kufahamu kuwa katika mchakato huo wa kuwapata wagombea hakukuwa na chuki wala uadui kwani CCM ina katiba nzuri inayokwenda kwa kanuni na taratibu nzuri.
Kwa upande wake kiongozi wa Umoja wa Wake wa Viongozi, Mama Asha Balozi ametoa pongezi kwa Mama Shein kwa ushirikiano wake mkubwa katika kufanikisha kongamano hilo pamoja na kueleza hatua zilizofikiwa na umoja huo.
Katika kongamano hilo mada mbali mbali zilitolewa ikiwemo “Wanawake Kutokata Tamaa”, aliyotolewa Balozi Amina Salum Ali, Waziri wa Biashara na Viwanda, Mada ya “Amani na Utulivu”,iliyotolewa na Sharifa Abeid Salum kutoka Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mada ya Tatu ilikuwa ni “Uzalendo na Mshikamano” iliyotolewa na Catherine Peter Nao Katibu wa Idara ya Uenezi Zanzibar.
Sambamba na hayo Kongamano hilo liling’arishwa na burudani mbali mbali kikiwemo kikundi cha Taarab cha “Big Star” cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku Dj Maarufu wa Zanzibar Kul Para akionesha mbwembwe zake katika tasnia ya muziki.