Rais Evariste Ndayishimiye, Rais Dkt.Magufuli wakubaliana mambo muhimu kuimarisha undugu baina ya Tanzania na Burundi
Rais wa Jamhuri ya Burundi,Évariste Ndayishimiye leo tarehe 19 Septemba, 2020 amefanya ziara rasmi ya siku moja hapa nchini ambapo amekutana mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli katika Mkoa wa Kigoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.John Pombe Magufuli akizungumza jambo na mgeni wake Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye wakati akimtambulisha kwa baadhi ya Mawaziri wa Tanzania katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma. (Ikulu).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt.John Pombe Magufuli akimpokea na kumkaribisha mgeni wake Rais wa Burundi, Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma leo tarehe 19 Septemba, 2020. (Ikulu).
Rais Ndayishimiye ambaye ameingia nchini kwa gari kutoka Burundi amepokelewa rasmi katika uwanja wa Lake Tanganyika Mjini Kigoma ambapo amepigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililoandaliwa kwa heshima yake.
Baada ya mapokezi rasmi,Rais Magufuli na Rais Ndayishimiye wamewasalimu wananchi wa Kigoma waliojitokeza katika mapokezi hayo na kisha wakaelekea eneo la Bangwe ambako wamefungua jengo la kisasa la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na baadaye wakaelekea Ikulu ndogo ya Kigoma ambako wamefanya mazungumzo rasmi, wamepata chakula cha mchana na kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama na mgeni wake Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye wakati wa heshma za nyimbo za Mataifa mawili zikipigwa katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma leo tarehe 19 Septemba, 2020. (Ikulu).
Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Ndayishimiye kwa kufanya ziara yake ya kwanza ya nje ya nchi hapa Tanzania na ameeleza kuwa huo ni uthibitisho kuwa Tanzania na Burundi sio tu ni nchi rafiki na jirani mwema, bali pia ni ndugu wa kweli.
Rais Magufuli amesema katika mazungumzo yake na Rais Ndayishimiye wamekubaliana kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi ikiwemo kuongeza biashara na uwekezaji, kuimarisha usalama, kuimarisha miundombinu hasa ya usafirishaji, kubadilishana uzoefu katika rasilimali ya madini na kukuza utalii.
Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye akikagua Gwaride la Heshma liliondaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma. (Ikulu).
Rais Magufuli amefafanua kuwa kati ya mwaka 2016 na sasa thamani ya biashara kati ya Tanzania na Burundi imeongezeka kutoka shilingi Bilioni 115.15 hadi kufikia shilingi Bilioni 201, na kwamba lengo ni kuongeza kasi na kiwango cha biashara ili nchi zote mbili zinufaike zaidi.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwasalimia wananchi waliofika kumpokea Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma. (Ikulu).
Amebainisha kuwa kutokana na dhamira hiyo wamekubaliana kuanza mara moja ujenzi wa kipande reli kuanzia Uvinza (Tanzania) – Msongati (Burundi) - Gitega (Burundi) ambacho baadaye kitaungana na reli ya kati ya kiwango cha kisasa (SGR) ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo mbalimbali ikiwemo madini aina ya Nickel ambayo yanapatikana Kabanga nchini Tanzania na Msongati nchini Burundi.
Rais Magufuli ameongeza kuwa Tanzania pia imechukua hatua madhubuti za kuimarisha biashara na Burundi zikiwemo kuimarisha bandari ya Dar es Salaam na kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (SGR) itakayotoka Dar es Salaam hadi Kigoma na kuunganishwa hadi Burundi, kuimarisha uwanja wa ndege wa Kigoma, kununua ndege zinazofanya safari zake moja kwa moja hadi Bujumbura na kuimarisha bandari ya Kigoma ili iwe bandari kuu katika Ziwa Tanganyika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye wakifungua kwa pamoja jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma leo tarehe 19 Septemba 2020. (Ikulu).
Juhudi nyingine ni kuimarisha barabara, kununua meli mpya 2 (moja ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 4,000 na nyingine yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400) na kukarabati meli za MV Liemba na MV Sangara ambazo zitarahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria katika ziwa Tanganyika, pia amempongeza Mhe. Rais Ndayishimiye kwa Burundi kufanikiwa kupata mkopo wa Dola za Marekani Milioni 23 kwa ajili ya kujenga bandari ya Bujumbura.
Aidha,Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Ndayishimiye kwa kuimarisha hali ya usalama nchini Burundi na ametoa wito kwa wakimbizi wa Burundi kurejea nchini kwao ili kuijenga nchi yao ambayo uchumi wake umeanza kukua na wadau mbalimbali wa maendeleo wameanza kurejesha uhusiano na nchi hiyo.
Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye akizungumza na Wananchi katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma. (Ikulu).
Kwa upande wake,Rais Ndayishimiye ambaye ameongozana na Mkewe Mama Angeline Ndayishimiye amemshukuru Rais Magufuli kwa kumkaribisha kufanya ziara yake ya kwanza nchini Tanzania na ameeleza kuwa anaiona Tanzania ni nyumbani (kwa Baba) na kwamba Burundi inaishukuru Tanzania kwa namna inavyoshirikiana nayo wakati wote na hususani kipindi cha machafuko na kuwapa hifadhi wakimbizi.
Rais Ndayishimiye amesema Burundi ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania ikiwemo kutumia bandari ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa inapitisha asilimia 95 ya mizigo yote ya Burundi na amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa namna alivyoleta mabadiliko nchini Tanzania ukiwemo mji wa Kigoma ambao umeboreshwa sana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.Rais Ndayishimiye amesema kwa sasa Burundi ni shwari, Warundi wengi wanarejea nchini humo na kwamba Serikali inawahimiza wananchi kujikita kufanya kazi ili kukuza uchumi na kuijenga Burundi.
Rais Ndayishimiye amerejea nchini Burundi. Unaweza kufuatilia kilichojiri katika video hapa chini.