Maalim Seif kuwezesha safari za Unguja hadi Pemba kwa saa 1, viwanda vya 'tomato' kuanzishwa

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema iwapo wananchi watampa ridhaa atahakikisha usafiri wa muda mfupi kwa kutumia boti za kasi baina ya Unguja na Pemba unapatikana ili wafanyabiashara wa visiwa hivyo kwenda sehemu moja na kurudi.

Maalim Seif ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mkanyageni Jimbo la Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za chama hicho katika Kisiwa cha Pemba.

Amesema, kama wananchi watampigia kura na kumuweka madarakani mara baada ya uchaguzi mkuu unaokuja atahakikisha anajenga bandari maalum katika eneo la Mkokotoni Unguja na Mkoani Pemba.

Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad akikagua shamba la Kikundi cha Green Base Group kilichopo Ziwani Wilaya ya Chakechake Pemba. (DIRAMAKINI).

“Lengo langu ni kuona wafanyabishara kutoka Pemba wanakuwa na uwezo wa kwenda Unguja na kurudi mara wanapomaliza shughuli zao na wa Unguja hivyo hivyo,"amesema Maalim Seif.

Amesema kuwa, akiwa Rais atahakikisha anagiza boti za kisasa ambazo zitatumia muda wa saa moja na nusu mpaka Unguja au Pemba.

Sambamba na hilo ameeleza kuwa, usafiri huo utaweza kusaidia watalii wanaokuja Unguja kuona rahisi kufika Pemba na kujionea vivutio viliopo.

“Watalii wengi wanafika Unguja, lakini hawafiki Pemba kutokana na kukosekana usafiri wa uhakika na wa kasi ,lakini katika utawala wangu miezi sita ya mwanzo hilo nitalitatuwa,”ameeleza Maalim Seif.

Ameeleza kuwa, kama utakuwepo usafiri huo utaweza kukuza maendeleo ya Pemba na Zanzibar kwa ujumla wake.

Ameeleza kuwa, kwa sasa bidhaa nyingi kisiwani Pemba zinaharibika kwa kukosa soko na kushindwa kusafirisha bidhaa zao kutokana na gharama kubwa ambazo hutozwa wanaposafirisha mazao yao.

Pia Maalim amesema, atazihamasisha kampuni za ndege kuleta ndege ambazo zitaweza kuchukuwa abiria kwa bei nafu tofauti na leo.

Amesema, kama nauli za ndege na boti zitakuwa chini baina ya Unguja na Pemba basi maisha ya mmoja mmoja na Zanzibar kwa ujumla yanawza kubadilika.

“Hata wawekezaji wanaweza kuongezeka kutokana na kuwepo uhakika wa safari na unafuu wa nauli," ameeleza Maalim Seif.

Sambamba na hilo Maalim Seif amesema anakusudia kujenga viwanja viwili vya Ndege vya Kimataifa ili iwe rahisi watalii kuingia Zanzibar.

Amesema kuwa, viwanja hivyo vitajengwa Pemba na Unguja ili iwe rahisi wawekezaji kuingia Zanzibar kuwekeza.

“Lengo langu ni kuibadilisha Zanzibar iwe ni nchi yenye kupiga hatua za kimaendeleo na maisha ya wananchi wake,"amesema.

Wakati huo huo Maalim Seif amesema anakusudia kujenga viwada vya kutengezea tomato za pakti ili kuwapunguzai mzigo kuharibikiwa na nyanya zao mashambani.

Akiwa katika shamba la nyanya la Green Base Group liliopo Ziwani Wilaya ya Chakechake, Maalim Seif amesema ni jambo la kusikitisha kuwa wananchi wajituma kwa ajili ya kujikomboa na umasikini lakini Serikali iliyopo madarakani haishahuliki kuwatafutia soko.

“Waziri wangu wa Kilimo atakuwa halali mpaka ahakikishe wazalishaji wamepata soko la uhakika,”ameeleza Maalim Seif.

Maalim Seif ameeleleza kuwa, kilio cha wazalishaji wengi Visiwani Zanzibar ni kukosa soko la uhakika la bidhaa zao.

Mapema mkulima wa nyanya katika kikundi hicho, Bi Naima Amour Ali amesema kutokana na kukosa soko la uhakika wa zao hilo hufikia mpaka nyingine kuharibikia shambani.

“Shamba letu alhamdulillah tunazalisha vizuri, lakini ugumu unakuja wakati wa kuuza bidhaa zetu kutokana uhaba wa wanunuzi kisiwan Pemba,”ameeleza Mkulima huyo.

Ameema katika shamba lao huvuna mara tatu kwa mwaka kutokana na juhudi zao binafsi na kudai jambo ambalo linawakatisha tamaa ni kukosa soko la uhakika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news