Majaliwa atikisa mkoani Mara, aahidiwa CCM kupewa mafiga matatu, awasisitiza Oktoba 28 siyo siku ya mzaha, Magufuli anatosha

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amemaliza ziara yake Mkoa wa Mara na kuwaeleza wananchi kwamba Oktoba 28, 2020 siyo siku ya mzaha, anaripoti Mwandishi Diramakini.

"Tarehe 28 Oktoba, 2020 siyo ya mzaha na wala siyo siku ya majaribio. Ni siku ya kuchagua kiongozi atakayetufaa, na huyo si mwingine bali ni Dkt.John Pombe Magufuli,"amesema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana Septemba 22, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Kibara wilayani Bunda mkoani Mara kwenye mkutano wa kuwanadi wagombea wa CCM uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Kibara.

Amesema, kiongozi wa nchi anayefaa kuchaguliwa ni yule anayeweza kusimamia rasilmali za Taifa. "Ni yule anayeweza kusimamia tunu za Taifa, siyo mnapata kiongozi halafu akipewa nchi anabadilisha hadi wimbo wa Taifa."

"Tunahitaji kiongozi anayeweza kupambana na rushwa, awe mtu wa kutetea watu wake wapate haki bila kuombwa rushwa. Huyo si mwingine bali ni Dkt.John Pombe Magufuli,"amesisitiza Majaliwa.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Mara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt.John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa Jimbo la kuwaombea kura Charles Kajege na Diwani wa Kibara, Bw. Nyanguli Mtesigwa na madiwani wengine wa jimbo hilo. Jioni hii anaingia mkoa wa Mwanza.

Akielezea umuhimu wa chama kuwa na Ilani ya Uchaguzi, Mheshimiwa Majaliwa amesema Chama Cha Mapinduzi kimeandaa ilani yake yenye kurasa 303 ikisimamia yale yaliyokuwemo kwenye ilani iliyopita ambayo ilikuwa na kurasa 236 na mengine mengi mapya.

"Watekelezaji wa hayo yote yaliyoainishwa kwenye Ilani ni hawa watatu ambao nawaombea kura leo. Namuombea kura Dkt.Magufuli ili akamilishe aliyoyaanza na atekeleze yaliyomo kwenye Ilani ya sasa. Ni lazima tumpatie mbunge na diwani wa CCM ili waweze kuzungumza lugha moja,"amesema Majaliwa.

Kuhusu uboreshaji kwenye sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa amesema zilitumika sh.bilioni 1.8 za kujenga hospitali ya wilaya hiyo na bado kuna sh.milioni 152 zilitolewa ili kuisaidia halmashauri kujenga zahanati.

Kuhusu sekta ya maji, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh.bilioni 6.2 zimetumika kukarabati na ujenzi wa miradi mbalimbali kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, ikiwemo uchimbaji wa visima virefu na vifupi, utengenezaji wa matenki ya kuvuna maji na uchimbaji wa mabwawa.

“Vijiji vilivyonufaika na miradi hii ni Nyatwali, Nyamuswa, Mgeta –Nyang’aranga, kinyabwiga, Bulamba na Kibara. Pia jumla ya shilingi milioni 90.1 zimetumika kwa ajili ya ukarabati na usafishaji wa pampu za mkono 67 na visima vitatu,”amesema.

Mapema asubuhi, akiwa Kata ya Kisorya, Mheshimiwa Majaliwa aliwaeleza wananchi hao kwamba Serikali ya CCM ina mpango wa kuboresha kituo chao cha afya kwa kuongeza wodi tatu za wanawake, wanaume na watoto.
Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Mwibara, Kata ya Kisorya Bunda, katika mkutano wa kampeni, Septemba 22, 2020. (PMO).

Pia amesema zimetengwa sh.milioni 550 za kuimarisha kituo hicho kwa kuongeza majengo ya jiko, chumba cha kufulia na chumba cha kuhifadhia maiti.

Kuhusu barabara, amesema kiasi cha sh. bilioni 2.9 kimetumika kutengeneza barabara za kuunganisha vijiji kwa vijiji, kukarabati sehemu korofi zilizoharibiwa na mafuriko, madaraja, makalvati na matengenezo ya kawaida.

Aidha, kuhusu umeme, amesema vijiji 77 kati ya 78 vina umeme isipokuwa kijiji kimoja tu cha Nafubu kilichopo kisiwani, ambacho amesema watapelekewa huduma ya umeme wa jua kwa vile siyo rahisi kupitisha nyaya za umeme majini.

MUSOMA

Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema sh. bilioni 25.3 zimetumika kuboresha barabara na mitaa ya Manispaa ya Musoma ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya mwaka 2015 -2020.

“Shilingi bilioni 18.7 zimetumika kujenga kilomita 14 za barabara kwa kiwango cha lami na kuweka taa za barabarani kupitia Programu ya Uboreshaji wa Miji (ULGSP) katika Manispaa ya Musoma na mradi umekamilika. Tunataka taa ziwake ili usiku uwe mchana, na mchana uwe mchana,”amesema.

Alitoa kauli hiyo jana jioni Septemba 21, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Musoma katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya Mara Sekondari, katika kata ya Nyamatare, wilayani Musoma, mkoani Mara.

Alisema kupitia Road Fund (Maintenance) kiasi kingine cha sh.bilioni 6.6 kilitumika kwa ajili ya kufungua barabara mpya, kufanya matengenezo ya kawaida na matengenezo ya sehemu korofi na kwamba miradi yote imekamilika.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Mara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Musoma Mjini, Bw. Vedasto Manyinyi, mgombea udiwani wa kata ya Nyamatare, Bw. Masumbuko Magesa na madiwani wengine wa manispaa hiyo.

“Ninawasihi wana Musoma msisite kumpigia kura Dkt. John Pombe Magufuli hata kama wewe ni mpenzi wa chama kingine kwa sababu yeye ndiye mleta maendeleo kwa nchi yetu,”alisema.

Akielezea mambo mengine yaliyotekelezwa chini ya Ilani hiyo, Mheshimiwa Majaliwa alisema “kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani” ililenga kumpunguzia mama kazi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji na badala yake atembee hatua chache kutoka bombani hadi nyumbani akiwa ameshika ndoo yake mkononi.

“Ili kuboresha huduma za upatikanaji wa maji kwenye mji wa Musoma, shilingi bilioni 46 zilitolewa kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji safi katika Manispaa ya Musoma ambao tayari umeanza kutoa huduma,”amesema.

Alisema sh.bilioni 18 zimetolewa kwa mradi wa kusambaza maji katika Manispaa ya Musoma na vijiji vitatu vya Musoma Vijijini na Butiama, ambapo kazi zinazofanywa ni ujenzi wa tenki la Bharima lenye ujazo wa lita milioni tatu; ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (Booster station) na ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kwenda kwenye tenki la Bharima (Rising main) lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 1.56.

Alizitaja kazi nyingine zilizofanyika kuwa ni ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kutoka kwenye tenki la Bharima kwenda kwa wananchi (Transmission main) lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 7.058; ufungaji wa pampu tatu zenye uwezo wa kusukuma mita za ujazo 175 kwa saa; ununuzi ya bomba za kusambaza maji kilomita 44.3 na ununuzi wa vifaa vya kutendea kazi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Mzee Stephen Wassira aliwataka wakazi wa Manispaa ya Musoma wakawapigie kura wagombea kutoka vyama vyenye ilani ya uchaguzi makini kama CCM.

“Tukisema mkapige kura, nendeni mkapige kura kwa wagombea na vyama vyenye Ilani ya Uchaguzi. Si kukupigia chama ili mradi ni safari tu ya kwenda kupiga kura. CCM inazo sera zake na ndiyo maana tunawaomba muwapigie kura wagombea wa CCM,”alisema.

“Hatuwezi kumpa mtu kura za urais kwa sababu tu tumekutana njiani. Rais ni Mkuu wa nchi, Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Majeshi. Tunamuombea kura Rais Magufuli kwa sababu amejaribiwa na ameweza.”

Akitoa mfano wa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Magufuli mkoani Mara, Mzee Wassira alisema ameweza kukamilisha ujenzi wa hospitali ya Kwangwa ndani ya miaka miaka mitatu, ujenzi ambao ulisimama kwa zaidi ya miaka 40.

Uamuzi wa kujenga ile hospitali ulianzishwa kwa azimio la TANU la mwaka 1974 na likathibitishwa na mkutano mkuu wa TANU mwaka 1974. Hapakuwa na bajeti ya ujenzi, lilikuwa ni suala la kujitegemea. Kwa hiyo, tulianza na michango ya soda ndiyo maana ujenzi wake, umechukua muda mrefu kukamilika,”alisema.

RORYA

Wakati huo huo, shule 151 za Wilaya ya Rorya mkoani Mara zikiwemo 120 za msingi na 31 za sekondari zimenufaika na mpango wa elimu bila malipo uliotekelezwa tangu 2015 hadi 2020.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amebainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Shirati kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa Obwere,Kata ya Mkoma wilayani Rorya, mkoani Mara.

Amesema sh.bilioni 3.3 zilitolewa kwa ajili ya shule za msingi 120 za kufanya ukarabati, masuala ya utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.

“Kwa upande wa shule za sekondari, shilingi bilioni 2.5 zilitolewa kwa shule 31 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule,”amesema.

Akielezea uboreshaji wa miundombinu ya shule ulivyofanywa kupitia Mpango wa Lipa Kutokana na Matokeo (EP4R) ulivyotekelezwa, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh.bilioni 1.2 zilitolewa kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa, vyoo na nyumba za walimu kwa shule za msingi.

Alizitaja baadhi ya shule za msingi zilizonufaika na mpango huo kuwa ni Mori, Nyanduga, Buchuri, Kondo, Saye, Masonga, Kyaro, Kitembe, Bubombi, Oliyo B, Dagopa, Nyabi, Ratia, Kotwo, Muchirobi, Manyara, Ochuna na Nuamaguku.

“Kwa upande wa shule za sekondari, zimetumika shilingi milioni 777.8 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwemo maabara, madarasa, mabweni na vyoo kwa shule za Bukama, Mirare, Ngasaro, Nyamunga, Buturi, Goribe, Nyathorogo, Nyamtinga na Waningo,”alisema.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Mara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Rorya, Bw.Jafari Chege, mgombea udiwani wa Kata ya Mkoma, Bw. Ayoi Musa Sonde na madiwani wengine wa wilaya hiyo.

Akielezea utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye sekta ya umeme, Mheshimiwa Majaliwa alisema vijiji 74 kati ya vijiji 87 vya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya vimepata umeme. Alivitaja vijiji vilivyobaki visivyo na umeme kuwa ni Thabache, Nyabikondo, Nyahera, Bugendi, Burere, Wamaya, Nyabiwe, Masike, Busanga, Nyihara, Kyanyamsana, Nyamusi na Oliyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news