“Hiki siyo kipindi cha kujutia maamuzi au cha kufanya majaribio ya uongozi. Chagua kiongozi mwenye uwezo wa kungoza nchi. Usimchague mtu tu hata kama ni mtoto wa dada yako.”
Kauli hiyo imetolewa jana jioni Septemba 19, 2020 na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata za Issenye na Natta waliojitokeza njiani kumlaki wakati akielekea Mugumu, Serengeti, mkoani Mara kuwanadi wagombea wa CCM.
“Tunataka kiongozi atakayelinda rasilmali za Taifa hili. Na huyo si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Magufuli. Tunataka kiongozi atakayeweza kuongoza nchi. Wewe mwanachama wa chama rafiki iwe ACT, CHADEMA, NCCR au CHAUMA, mchague Dkt. John Pombe Magufuli awe Rais kwa sababu maendeleo hayachagui chama,” alisema.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia mikutano hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Serengeti, Bw. Amsabi Jeremiah Mhimi na wagombea udiwani wa kata za Issenye na Natta, Bw. Mosi James Nyarobi na Bw. Juma Porini.
Akielezea ni kwa nini anawaomba kura wananchi wa vyama vyote bila kujali itikadi zao za kisiasa, Mheshimiwa Majaliwa alisema: “Ni kwa sabau tunatafuta kiongozi wa nchi. Uongozi wa nchi unataka mtu mwenye busara mweledi, mchapakazi na mwenye nia ya kuleta maendeleo kwa Watanzania, na huyu si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.”
Alisema moja ya sifa za Rais wa nchi ni lazima awe na uwezo wa kulinda tunu za Taifa na moja ya tunu hizo hizo ni amani. “Mgombea urais anayeweza kati ya wote hawa niliowaona, ni Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Tarehe 28 Oktoba ikifika, nenda kampigie kura,” aliongeza.
Akielezea mambo yaliyofanyika kwenye sekta ya afya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilihakikisha Watanzania hawalipi gharama nyingi kwa ajili ya matibabu na ndio maana iliboresha huduma hiyo kuanzia ngazi ya zahanati ili wananchi wapate huduma za afya kwa karibu zaidi.
Katika wilaya ya Serengeti, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 1.7 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo ambapo majengo ya huduma ya mama na mtoto, utawala, kusubiria wagonjwa, OPD na njia ya waendao kwa miguu yalijengwa. Alisema majengo yote hayo yamekamilika na yanatumika.
“Vilevile, shilingi milioni 429 zimetolewa kwa ujenzi wa kituo cha afya Natta, ujenzi wa wodi ya wazazi, wodi ya watoto, maabara, jengo la X-Ray, nyumba ya kuhifadhia maiti na nyumba ya watumishi (6 in 1). Ujenzi umekamilika na majengo hayo yanatumika,” alisema.
“Kuhusu ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, wilaya hii ilipokea shilingi bilioni 1.5. Kila mwezi, zimekuwa zikiletwa fedha za dawa za wastani wa shilingi milioni 30.9,” amesema.
Alisema Halmashauri ilipewa gari moja la kubebea wagonjwa ambalo lilipelekwa kwenye kituo cha afya cha Natta na linafanya kazi.
Wakati huo huo, shule 156 za wilaya ya Serengeti zikiwemo 122 za msingi na 34 za sekondari zimenufaika na mpango wa elimu bila malipo kwa kupatiwa sh. bilioni 6.2 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Hayo yamebainishwa jana jioni Septemba 19, 2020 na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na wakazi wa Mugumu, wilayani Serengeti, mkoani Mara katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Sokoine.
Akiwafafanulia mambo yaliyofanywa na Serikali ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya miaka mitano, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 2.9 zilitolewa kwa shule za msingi 122 kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.
Kwa upande wa elimu ya sekondari, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 3.3 zilitolewa kwa shule 34 ili kulipia fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.
Akielezea mpango mwingine ambao umezinufaisha shule nyingi za wilaya hiyo, Mheshimiwa Majaliwa alisema mfumo wa uboreshaji wa miundombinu ya shule wa Lipa Kutokana na Matokeo (EP4R) uliotekelezwa tangu 2015 hadi 2020 umewezesha sh. bilioni 2.7 zitolewe kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa, vyoo na nyumba za walimu wa shule za msingi.
“Shilingi bilioni 1.7 zilizotolewa awali na awamu ya pili zikatolewa shilingi bilioni moja. Baadhi ya shule za msingi zilizonufaika na fedha hizo ni Wageti, Nyamakendo, Moningori, Masangura, Maburi, Kitunguruma, Itununu, Mchuri, Merenga, Mesanga, Miseke, Busawe, Musati, Monuna, Nyamburi, Nyiberekera, Motukeri, Kemugongo, Nyansurumunti, Mugumu na Nayaigabo,” alisema.
Alisema shule za sekondari zilipatiwa sh. milioni 3.076 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwemo maabara, madarasa, mabweni na vyoo. “Katika awamu ya kwanza zilitolewa shilingi bilioni 2.1 na awamu ya pili zikalipwa shilingi milioni 976.2.”
Alizitaja shule hizo kuwa ni Mugumu, Kitunguruma, Busawe, Nyamoko, Natta, Robanda, Serengeti, Ring’wani, Machochwe, Rigicha, Manchira, Mama Maria Nyerere, Ikongoro, Nagusi, Dkt. Omari Ali Juma na Nyambureti.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia mkutano huo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli na kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Serengeti, Bw. Amsabi Jeremiah Mhimi, mgombea udiwani wa kata ya Stendi Kuu, Bw. Steven Mapancha na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Serengeti.
Kuhusu maji safi na salama, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 3.4 zimetumika kukarabati na kujenga miradi mbalimbali wilayani Serengeti, ikiwemo vijiji vya Natta, Motukeri, Makundusi, Nyamakobiti, Majimoto, Musati, Kebanchabancha, Kutunguruma, Kenyana na Nyamitita.
“Vilevile, shilingi milioni 62.5 zimetumika kwa ajili ya uchimbaji wa kisima kimoja kwenye kijiji cha Makundusi na ukarabati wa visima vya pampu za mikono kwenye vijiji 19,” alisema.
Kuhusu huduma ya umeme, Mheshimiwa Majaliwa alisema jumla ya vijiji 69 kati ya vijiji 78 vya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti vimepata umeme na vijiji vilivyobaki visivyo na umeme ni tisa tu ambavyo vitapata kwa sababu mkandarasi yuko kazini.