MAJALIWA: MIRADI YA MAJI BUSEGA IMETUMIA BILIONI 3.7/-,EP4R IMEZINUFAISHA SHULE NYINGI BARIADI

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema sh. bilioni 3.7 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika wilaya ya Busega.

Ametoa kauli hiyo leo mchana Septemba 18, 2020 kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata za Mkula na Lamadi, wilaya ya Busega, mkoani Simiyu wakati akiwa njiani kuelekea wilayani Bunda mkoani Mara.

Mheshimiwa Majaliwa amesema, fedha hizo zimetumika kujenga mradi wa maji bomba katika kijiji cha Lukungu ambao tayari umekamilika.

“Pia fedha hizo zilitumika kufanya ukarabati wa chanzo cha maji katika mradi wa maji wa Kalemela-Mkula ambao nao tayari umekamilika.”

Ameitaja miradi mingine kuwa ni mradi wa maji bomba Kiloleli unaohudumia vijiji vitatu vya Ihale, Ijitu na Yitwimila B ambao pia umekamilika.

Amesema, fedha hizo zimetumika kufanya upanuzi wa mradi wa maji Lamadi (Kalago na Mwabayanda) ambao umefikia asilimia 50; upanuzi wa mradi wa maji Nyashimo ambao umefikia asilimia 10; ujenzi wa mradi wa maji Mkula sekondari ambao umefikia asilimia 60 na mradi wa maji Bushgwamhala ambao umefikia asilimia 100.

Kuhusu umeme, Mheshimiwa Majaliwa amesema kati ya vijiji 59, vijiji 53 vimeshapelekewa huduma ya umeme, na vijiji sita bado havina umeme. Amesema vijiji ambavyo havina umeme, vipo kwenye mpango wa kupelekewa umeme.

Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa amesema ili kuboresha miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo mpya, sh. bilioni 2.3 zimetolewa kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Amesema fedha zilizotolewa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara zilihusisha barabara za Mwamanyili – Busami; Masanza Sec. School - Sayaka Road; Nyamikoma - Busega na Lamadi Sec.School - Suti Moja.

Amezitaja barabara nyingine kuwa ni Masanja-Ashico Petroli Road; Malili- Mwamigongwa-Ng'wang'wenge; Nyang'haya-Kasoli na Ngong'ho-Ndono Petrol Station.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Busega, Bw. Simon Songe na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Busega ambao wawili kati yao wamepita bila kupingwa akiwemo mgombea udiwani wa Mkula, Bw. Godfrey Kalango.

Wakati huo huo shule 28 za wilaya ya Bariadi zikiwemo 11 za msingi na 17 za sekondari zimenufaika na mfumo wa uboreshaji wa miundombinu ya shule wa Lipa Kutokana na Matokeo (EP4R) uliotekelezwa tangu 2015 hadi 2020.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa aliyasema hayo jana Alhamisi, Septemba 17, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Nkololo, wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nkololo 'A'.

Akielezea utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wakazi hao, Mheshimiwa Majaliwa alisema awali zilitolewa sh. bilioni 2.3 na Septemba, mwaka huu zimetolewa sh. milioni 457 ili kukamilisha uwekaji miundombinu ya nyumba za walimu, madarasa na matundu ya vyoo katika shule za msingi za Halawa, Kilabela A, Tunge, Mwauchumu, Bukiliguu, Byuna, Chungu cha bawawa, Damidami, Masewa C, Mwashagata na Banemhi zilizoko wilayani humo.

“Kwa upande wa shule za sekondari, shilingi bilioni 1.07 zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya nyumba za walimu, madarasa, maabara, majengo ya utawala na matundu ya vyoo kwa sekondari za Dutwa, Mwantimba, Gegedi, Miswaki, Mwamlapa, Nkololo, Nyasosi, Nyawa, Sapiwi, Banemhi, Gasuma, Igaganulwa, Ikinabushu, Itubukilo, Mwadobana, Sakwe na Nkindwabiye.”

Kuhusu mpango wa elimu bila malipo, Mheshimiwa Majaliwa alisema shule za msingi 79 zilipatiwa shilingi bilioni 3.12 kwa ajili ya ukarabati wa majengo, masuala ya utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.

Alisema shule za sekondari 23 zilipatiwa shilingi bilioni 1.43 kwa ajili ya kulipia fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.

Akielezea miradi ya barabara, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 3.2 zimetolewa kupitia TARURA kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi, na ujenzi wa barabara zenye urefu wa km. 246 ambazo zimefanyiwa matengenezo kwa kiwango cha udongo, km. 37.6 kwa kiwango cha molamu. Pia, makalvati 108 yamejengwa.

Alizitaja barabara zilizofanyiwa matengenezo hayo kuwa ni za Ikungulyabashashi – Ditima; Byuna - Nkindwabiye - Halawa; Igegu - Matongo Gibishi - Halawa; Dutwa- Gilya - Mwauchumu; Nyakabindi - Mwadobana - Gasuma; Kasori Centre - Kasori Ginnery na Nyamswa - Mwasubuya - Bwawani.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Bariadi, Injinia Kundo Mathew, mgombea udiwani wa kata ya Nkololo, Nyamwela Sinda na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Bariadi waliokuwepo kwenye mkutano huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news