Majaliwa:Chagueni viongozi wenye mtazamo mmoja

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Bariadi wachague viongozi wenye mtazamo mmoja ili kuleta maendeleo ya haraka.

"Ili upate uongozi unaoweza kuleta maendeleo, usichanganye viongozi wenye mitazamo tofauti. Ni vema tukaweka viongozi wanaozungumza lugha moja," amesema. Ametoa wito huo leo Septemba 17, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Nkololo Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nkololo 'A'.
Ametumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt.John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa Jimbo la Bariadi,Mhandisi Kundo Mathew, mgombea udiwani wa Kata ya Nkololo, Nyamwela Sinda na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Bariadi waliokuwepo kwenye mkutano huo.

Akizungumza na wakazi hao, Mheshimiwa Majaliwa amesema Chama Cha Mapinduzi kimetekeleza ahadi yake ya kuboresha miradi ya maji kwa kutoa sh.bilioni 3.2 zilizotumika kwenye vijiji vya Nkololo, Igaganulwa, Mwamlapa, Kasoli, Sengerema, Sanungu, Mahina, Nyangokolwa Masewa, Nyakabindi na Bupandagila.

"Serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi ilifanya ukarabati wa visima 120 na kununua pampu 64 na kuzifunga kazi ambayo imefikia asilimia 90 ikiwa ni kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais ya kumtua Mama ndoo kichwani ambayo ilikuwepo kwenye Ilani ya 2015-2020."

Kwenye sekta ya afya, amesema ujenzi wa vituo vya afya unaendelea na vituo hivyo vina uwezo wa kupima magonjwa yote, kufanya upasuaji na kutoa huduma kwa akinamama wajawazito. "Nia yetu ni kuvisambaza hadi huko wananchi waliko, Rais wetu anataka wananchi wasipate shida ya kulipa nauli kufuata huduma za afya."

Akielezea yaliyofanyika chini ya Ilani ya CCM iliyopita, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh.bilioni 1.8 zimetolewa kwa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambalo sasa linatumika na majengo ya utawala, famasi, kufulia, maabara, mionzi, wodi ya wazazi ambayo yapo katika hatua ya ukamilishaji ya kuweka milango.

Amesema sh.milioni 450 zimetolewa kwa ujenzi wa kituo cha afya Byuna ambacho kina wodi ya wazazi, maabara, nyumba ya kuhifadhia maiti na nyumba ya mtumishi na tayari kinafanya kazi.

Kuhusu ujenzi wa zahanati, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh.milioni 150 zimetolewa na kukamilisha ujenzi wa wodi za wazazi katika zahanati za Sakwe, Igegu, Dutwa, Mwasinasi na Ikungulyambesi.

Kuhusu ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh.bilioni 2.2 zimetolewa kwa ajili ununuzi wa dawa na vifaa tiba ambapo fedha kwa wastani fedha iliyokuwa inatolewa kila mwezi ni sh. milioni 37.

“Tumepeleka magari ya kubeba wagonjwa kwenye Hospitali ya Wilaya Dutwa (moja) na Kituo cha Afya cha Byuna (moja),"amesema.

Mapema, mbunge aliyemaliza muda wake, Andrew Chenge aliwataka wakazi wa Bariadi waendelee kuziamini sera za CCM sababu ndiyo zinazoaminika na zinatekelezeka.

"Wana Bariadi tuhakikishe tarehe 28 mwezi ujao tunafanya kazi ya uhakika kwa kuchagua viongozi waliosimamishwa na CCM tupate mafiga matatu ili maendeleo ya wilaya yetu yaende kwa kasi," alisisitiza.

Aliwaombea kura Dkt. John Pombe Magufuli, Mhandisi Kundo Mathew na madiwani 24 kati ya 31 wa wilaya ya Bariadi kwa sababu wagombea saba wameshapita bila kupingwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news