MAJALIWA:SERIKALI IMETEKELEZA MIRADI YA BILIONI 577. 53/- JIJINI ARUSHA

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa kampeni za CCM kwenye uwanja wa Relini, jijini Arusha, Septemba 5, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imetoa sh. bilioni 577.53 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara jijini Arusha.

Ameyasema hayo leo alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Relini jijini Arusha baada ya kumuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge jimbo la Arusha, Mrisho Gambo na wagombea udiwani wa CCM.

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Zuwena Mohammed maarufu  kwa jina la Shilole akiimba katika mkutano wa kampeni za CCM uliohutubiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  kwenye uwanja wa Relini jijini Arusha Septemba 5, 2020. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu).


Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa kampeni za CCM kwenye uwanja wa Relini, jijini Arusha, Septemba 5, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 

Waziri Mkuu amesema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.3 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Arusha ambapo jengo la wagonjwa ya nje (OPD) limekamilika na ujenzi wa jengo la akina mama unaendelea.

“Jumla ya shilingi bilioni 1.5 zimetolewa kwa Jiji la Arusha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya vya Muriet, Kaloleni na Moshono ambapo ujenzi wake umekamilika na wananchi wanaendelea kupatiwa huduma,"amesema.

Waziri Mkuu amesema mbali na ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, pia Serikali imetoa shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa kipindi cha 2015/2016–2019/2020 katika jiji la Arusha, upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 98.

Amesema, Serikali imetoa shilingi bilioni 2.14 kwa ajili ya kugharamia shughuli za ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu katika shule za msingi 48 jijini Arusha. “Shilingi bilioni 4.68 zimetolewa katika shule za sekondari 29 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule.”

Pia, Waziri Mkuu amesema shilingi bilioni 1.03 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa na vyoo kwa shule mbalimbali za msingi jijini Arusha ikiwemo Olasiti, Daraja II, Oloirien na Sokoni I.

Akizungumzia kuhusu shule za sekondari, Waziri Mkuu amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 4.68 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, mabweni, vyoo na majengo ya utawala ikiwemo shule za Suye, Muriet, Lemara, Sorenyi, Arusha na Korona.

“Jiji la Arusha linakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, hivyo Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 520 kwa ajili ya mradi wa majisafi jiji la Arusha ambao utahudumia Jiji lote la Arusha. Utekelezaji wake umefikia asilimia 52.”

Amesema shilingi bilioni 38.4 zimetolewa kupitia TARURA katika kipindi cha 2015/2016 – 2019/2020 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami na madaraja kwa jiji la Arusha ukiwemo ujenzi wa barabara ya Oljoro – Muriet yenye urefu wa km. 2.8. Barabara nyingine ni za Kisongo Bypass km. 3.4, barabara ya Sokoine –Muriet Meidimu urefu wa km. 8.5, barabara ya Njiro km. 2.8, barabara ya Ngarenaro km. 4.1 na ujenzi wa barabara ya Sombetini km. 2.0.

“Barabara ya Arusha – Holili/Taveta. Ujenzi wa sehemu ya barabara kutoka Sakina hadi Tengeru, Km14.1 na ujenzi wa barabara ya mchepuko wa kusini (Southern-bypass), Km 42.41 ambazo zinajengwa na TANROADS (Wakala wa Barabara Tanzania) zitahudumia Jiji lote la Arusha na Halmashauri za Wilaya Arusha na Meru,”amesema.

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Arusha kumchagua Rais Dkt. Magufuli kwa kuwa ana uwezo mkubwa wa kusimamia mambo yanayowagusa wananchi na ametekeleza vyema Ilani ya CCM ya mwaka 2015 kwa vitendo na sasa anakuja na Ilani mpya iliyosheheni mambo mengi ya maendeleo.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano Watanzania wakiwemo wakazi wa mkoa huo wa Arusha wamenufaika kutokana na miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo imejengwa nchini ikiwemo ufufuaji wa usafiri wa treni ya Dar es Salaam hadi Arusha ambao ulikuwa umesimama kwa takribani miaka 30.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news