MAJALIWA:WANAMONDULI HAKIKISHENI CCM INASHINDA KWA KISHINDO

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amevunja makundi ya wanachama wa CCM walioomba uteuzi wa kuwania ubunge katika jimbo Monduli mkoani Arusha na kuwataka washirikiane katika kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa  na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimnadi Mgombea Ubunge Jimbo la Monduli, Fred Lowassa wakati alipozindua Kampeni za CCM wilayani Monduli, Septemba 2, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo amewaomba wakazi wa wilaya ya Monduli mkoani Arusha na Watanzania wote bila kijali itikadi zao wamchague Rais Dkt John Pombe Magufuli ili aendeleze kazi ya kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Septemba 2, 2020) wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Monduli, Arusha kwenye mkutano wa kampeni za CCM kumuombea kura Rais Dkt. Magufuli pamoja na wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani wa CCM.

“Kazi iliyonileta hapa ni kuwaomba kura wana Arusha na wanaMonduli naomba kura zenu zote bila ya kujali itikazi za vyama vyenu tumpigie kura Mheshimiwa Rais Magufuli na mgombea ubunge Fredrick Lowassa na wagombea wote wa udiwani kupitia CCM.”`
Mgombea Ubunge Jimbo la Monduli kwa tiketi ya CCM, Fred Lowassa (kulia) akipongezwa na Mbunge wa jimbo hilo aliyemaliza muda wake Julius Kalanga wakati Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozindua Kampeni za CCM Jimbo la Monduli kwenye Uwanja wa Barafu, Mto wa Mbu, Septemba 2, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Amesema wananchi wanajua kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli, hivyo amewaomba wamchague tena kwa kuwa miradi mikubwa ya kimkakati aliyoitekeleza kwenye maeneo mbalimbali nchini imegusa wananchi wengi.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 imeweka msisitizo kwa Serikali kuleta mageuzi ya utalii, kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi.

“Tutahakikisha uzalishaji unaongezeka katika sekta ya mifugo, utalii na uvuvi kwa ajili ya kuongeza tija katika kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuchochea maendeleo ya uchumi, hasa katika sekta za viwanda na huduma za jamii. Fugeni kisasa mpate faida na Serikali ya CCM itaendelea kuwaunga mkono.”

Amesema, tayari vijana wengi wamenufaika kupitia sekta hizo, hivyo ni lazima Serikali iendelee kuziboresha zaidi. Pia Serikali imepanga kuongeza idadi ya watalii wanaoingia pamoja na kuongeza pato litokanalo na sekta hiyo.



Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news