Makachero wa TAKUKURU, Kibiti waokoa mamilioni ya fedha za wakulima wa korosho

OFISI ya Mkuu wa Wilaya Kibiti na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo imeokoa kiasi cha sh. milioni 44,054,040 za wakulima wa korosho wa vyama vya ushirika Mwambao Amcos na Ruaruke Amcos vya Wilaya ya Kibiti za mauzo ya korosho msimu wa mwaka 2019/2020.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani,Gullam Hussein Kiffu akitoa taarifa ya kuokoa fedha za wakulima wa korosho Kibiti amesema, korosho za vyama hivyo ziliuzwa katika mnada wa Januari 24, 2020 kwa Kampuni ya RV. EXPORT zikiwa jumla ya kilogramu 157,591 ambapo baada ya korosho kuuzwa mnunuzi alichukua jumla ya kilo 71,845 na kuacha kilo 85,746.

Mkuu huyo amesema, korosho zilizobaki ziliendelea kukaa ghalani hadi TAKUKURU na ofisi ya mkuu wa wilaya ilipofuatilia suala la wakulima wasiolipwa haki zao wapate.
Amesema, baada ya ufuatiliaji kuanza ilibainika kuwa mnunuzi wa korosho alikuwa ameshalipa fedha CORECU kwa ajili ya wakulima wa Mwambao na Ruaruke na baada ya fedha hizo kulipwa hazikuwafikia wakulima walengwa badala yake CORECU walizipeleka kwa wakulima wengine wasiohusika.

"Suala hili liliendelea kufuatiliwa na Ofisi ya TAKUKURU na tarehe 28 mwezi wa 8, 2020 kikao cha pamoja ambacho kilishirikisha ofisi ya mkuu wa wilaya, TAKUKURU, ofisi ya Mkurugenzi na viongozi wa Amcos husika tulikaa kwa pamoja na ndipo ilipoamuliwa kwamba CORECU wawalipe wakulima fedha zao ndani ya siku 14,"amesema Kiffu na kuongeza kuwa;

"Napenda kuwajulisha kuwa CORECU wametekeleza kilichoagizwa na wamelipa kiasi cha shilingi 44,054,040 ambapo mnaziona hapa na nyingine tayari tumeshawalipa wakulima,"amesema.

Kiffu ameongeza kuwa, zoezi la ufuatiliaji fedha za wakulima wa korosho lilianza tangu mwezi Novemba 2019 ambapo hadi leo shilingi milioni 300,920,780 zimeokolewa na kulipwa kwa wakulima ambao walikuwa hawana tena matumaini ya kupata fedha zao.

Ametoa wito kwa viongozi wa AMCOS na CORECU kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa ili kuepusha hujuma kwa mazao ya wakulima wanyonge ambao wanatumia gharama kubwa kwenye madawa ,lakini baada ya mavuno fedha zao au mauzo yao yanahujumiwa na watu wachache.

"Lakini pia makampuni ya ununuzi wa mazao ya wakulima wa Kibiti nawaasa kuacha ujanja ujanja wa kuwadhulumu wakulima badala yake fuateni sheria, kanuni na taratibu kwani mtajikuta mnaingia katika matatizo ambayo yatayumbisha biashara zenu,"amesema Kiffu.

Amesema,TAKUKURU inataka kuwaona wananchi wanyonge wa chini wakitendewa haki na pia wakipata haki zao kwa wakati jambo ambalo Rais Dkt.John  Magufuli amekuwa akilipigia kelele kila siku na kulitekeleza kwa vitendo.

Awali, Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Kibiti, Anna Shine amesema walipokea malalamiko kutoka kwa vyama viongozi wa Ruaruke Amcos na Mwambao Amcos kuwa baadhi ya wakulima wanadai fedha zao na walienda hadi ofisi ya mkuu wa wilaya na wao walianza kushughulikia madai hayo.

"Korosho ziliuzwa kwa Kampuni ya RV ambaye alizibeba nusu nyingine akaziacha kwa madai ya changamoto ya barabara na ubovu wa korosho. Ambapo wakulima walikubali wakatwe kufidia ubovu wa barabara kwa kutoa shilingi 80 kwa kila kilo ya korosho, fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ya CORECU, lakini CORECU wakijua walichokifanya, walichukua fedha hizo hizo kuchepushwa na kupeleka kwa wakulima wengine ambao si walengwa,"amesema Anna.

Hata hivyo, amesema walikaa pamoja na uongozi wa chama kikuu cha msingi Mkoa wa Pwani CORECU na Amcos jitihada zilizosaidia kubaini fedha zilipopelekwa ambazo zimerudishwa na kupewa wakulima. walengwa.

Amesema, wanachi wa Kibiti waitumie vizuri ofisi yao kwani wananchi wengi wamepata haki zao kupitia ofisi hiyo.

"Tutaendelea kuchapa kazi kwa kasi hii hii ili tuweze kutokomeza rushwa na hujuma wanazofanyiwa wakulima wetu wa Kibiti,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news