MAKALA MAALUM; Kassim Majaliwa anavyoendesha kampeni za kisayansi, kuunganisha na kuwapa mwanga Watanzania, Kilimanjaro yang'aa

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wasichague viongozi kwa kutumia vigezo vya udini, ukabila, itikadi za vyama na badala yake wachague viongozi watakaokuwa tayari kushirikiana nao katika kuboresha maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

 

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo Septemba 8, 2020 wakati akimuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Hai, Saasisha Mafuwe na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Masama Kusini kwenye uwanja wa Kwa Sadala wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.

Wananchi wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (juu) wakati alipohutubia mkutano wa kampeni, Kwasadala wilayani Hai, Septemba 8, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Ndugu zangu Watanzania, ndugu zangu wanaHai na wanaKilimanjaro mnatambua uwezo na uelewa mkubwa alionao Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli wa kutambua na kuona nini Watanzania wanahitaji, nawaomba siku ya kupiga kura itakapofika tujitokeze kwa wingi bila kujali itikadi zetu tumpigie kura nyingi ili akaendeleze miradi ya maendeleo aliyoianzisha.”

 

Amesema, wakati umefika kwa wakazi wa Hai kuchagua kiongozi mwenye kujali na kutambua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi na kamwe wasikubali kupiga kura kwa ushabiki au kufuata mkumbo. “Mchague Rais Dkt. Magufuli kwa nafasi ya urais na Saasisha nafasi ya ubunge pamoja na wagombea udiwani wote wa CCM.”

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Magufuli ni kiongozi anayetokana na Chama Cha Mapinduzi chenye utaratibu wa kuratibu miradi yote inayotakiwa kutekelezwa katika maeneo yote nchini kupitia ilani ya uchaguzi na kina mipango mizuri ya kuboresha maendeleo ya wananchi.

 

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo kupitia mradi mkubwa wa maji unaojengwa kwa sh. bilioni 520 kutoka Machame hadi Arusha. Visima vimekamilika kuchimbwa na usambazaji wa mabomba umeanza.

 

“Katika mradi huu wananchi wa Hai walio katika kilomita 12 kushoto na kulia kando kando ya maeneo ambayo bomba la maji litapita tutahakikisha Mamlaka ya maji AWSA inaweka matanki kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi katika ukanda wa chini.”

Amesema sh. bilioni 3.3 zimetumika kukamilisha mradi wa ujenzi na upanuzi wa skimu ya maji LOSAA – KIA. Maeneo yanayonufaika ni pamoja na kata ya Masama Magharibi, Masama Kati, Masama Kusini na kata ya KIA.

Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. milioni 844 zimetumika kukamilisha ukarabati na ujenzi wa mifereji ya maji katika skimu za Nsanya, Musa Mwinjanga na Kikavu Chini.Skimu ya Uroke – Bomang’ombe imekamilika na inahudumia maeneo ya Machame Uroki, Kwa Sadala, Kware, Romu na Mji wa Hai.

Kwa upande wao, wananchi wamesema watahakikisha wanawachagua wagombea wa CCM kwa sababu katika kipindi cha miaka 15 walichokuwa wakichagua viongozi wa upinzani hakuna kitu chochote walichokifanya cha maendeleo katika wilaya yao.

 

Miongoni mwa wananchi hao Betha Massawe amesema Rais Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi ya maendeleo ikiwe kufufua usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam hadi Arusha usafiri ambao ulisimama kwa miaka 30 jambo ambalo hadi leo haamini anaona kama ndoto.

 

Mkazi mwingine wa Hai, David Kiseyi amesema katika uchaguzi wa mwaka huu wamejipanga kuchagua viongozi kutoka Chama Cha Mapinduzi kwa sababu wamekuwa wakiwachagua viongozi wa upinzani bila ya faida yoyote. “Rais Dkt Magufuli ameonesha upendo mkubwa kwetu kwa kutuletea miradi ya maendeleo kwetu sasa tunakwenda kuacha ushabiki na tutachagua viongozi watakaotuletea maendeleo. Watu wa Hai tuache ushabiki tuchague maendeleo.”

 

"Huyu Mbunge ametufanya sisi kama watoto anakuja tunampa kura kwa ahadi zake nyingi na anapopata hutumuoni tena anakimbilia Dar es salaam na Dodoma utafikiri wananchi wa huko ndio wamemchagua sasa hatupo tayari kudanganywa na maneno ya uongo ni bora akaanza kukusanya virago vyake" alisema Halima Mushi mkazi wa Machame.

 

 SIHA

 

Wakati huo huo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Watanzania wana kila sababu ya kumchagua Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu kwa sababu ni kiongozi makini, shupavu, mbunifu na mwenye uwezo wa kusimamia vizuri rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wote.

Naibu Waziri na Mkuu wa Mkoa Mstaafu, Aggrey Mwanri na  mgombea ubunge wa CCM wa jimbo la Siha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Godwin Mollel wametamka hadharani kuwa  watashirkiana katika kampeni ili kuhakikisha kwamba CCM inapata ushindi mnono katika jimbo hilo. Pichani, Mwanri (kulia) akimnadi Dkt. Mollel  badda wanasiasa hao kutamka hayo katika mkutano wa kampeni uliohubiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kijiji cha Matado wilayani humo, Septemba 8, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema katika kipindi cha miaka mitano ya awamu ya kwanza ya uongozi wake, Rais Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini na yamewanufaisha Watanzania wote wakiwemo na wakazi wa wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

 

Ameyasema hayo leo alipokuwa akimuombea kura Rais Dkt. Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Siha Dkt. Godwin Mollel na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Matadi kata ya Ndemet wilaya ya Siha, Mkoani Kilimanjaro.

 

Amesema, Watanzania wanatakiwa wamchague Rais Dkt. Magufuli ili aweze kuwaongoza katika kusimamia vizuri matumizi ya rasilimali za Taifa kwa ajili ya maendeleo na kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini. Amesema Tanzania ni nchi tajiri yenye uwezo wa kuwaletea wananchi wake maendeleo bila ya utegemezi, hivyo wachague viongozi makini kwa manufaa ya Taifa.

 

“WanaSiha wote nimekuja hapa kwenu leo nina kazi moja tu ya kumuombea kura mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM, Rais Dkt. Magufuli ambaye ni kiongozi imara, mzalendo na mchapakazi, mgombea ubunge wa jimbo la Siha Dkt. Mollel na wagombea udiwani wote wa CCM katika wilaya hii. Ikifika siku ya kupiga kura tuhakikishe tunawachagua.”

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa lazima wananchi waamini kwamba uongozi unatoka kwa Mwenyezi Mungu na Rais Dkt. Magufuli ameletwa na Mwenyezi Mungu, hivyo amewaomba wampe ridhaa ya kuongoza katika kipindi cha miaka mitano mingine ili aendeleze kazi za maendeleo alizozianza.

 

“Nawasihi inapofika siku ya kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu tunapotumia haki ya msingi ya kidemokrasia, tukamchague Rais Dkt. Magufuli kwa sababu ni kiongozi anayejali maslahi ya Watanzania wote na ni kiongozi anayeweza kujua nchi inawakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara ambao kila mmoja anatakiwa afanye shughuli zake kwa uhuru bila ya kusumbuliwa.”

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi wa Siha kuwa Serikali itayarudisha mashamba yote ya Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU) yanayomilikiwa kinyemela na watu wachache kwa manufaa yao binafsi

 

“Kuna watu wamejimilikisha mahekari ya mashamba ya KNCU ambayo ni mali zenu, nawahakikishia tutawanyang’anya na kuyarudisha kwenu ili atakayelima alime, atakayefuga afuge”

 

Amesema KNCU ni mali ya wananchi (wanaushirika) na kwamba Serikali imefanya kazi kubwa ya kurudisha hadhi ya ushirika katika kipindi cha miaka mitano, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani waliohusika kufanya ubadhirifu katika vyama hivyo na itaendelea kurejesha mali zote kwa wananchi ili wafanyie shughuli za maendeleo.

 

Akizungumzia upatikanaji wa nishati ya umeme wilayani Siha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kati ya vijiji 60 vilivyopo Siha vijiji vyenye umeme ni 58 na viwili tu ndio havina umeme na kwamba navyo vitaunganishwa umeme, amewaomba wakazi wake waendelee kuwa na subira.

 

Amesema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Rombo. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.

 

Pia Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali yao.

 

 

ROMBO

    

Jana Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali imejipanga kuendeleza na kuimarisha sekta ya viwanda nchini ili kukuza uchumi na kumaliza tatizo la upatikanaji wa ajira hususani kwa vijana.

 

Amesema, sekta ya viwanda ndiyo msingi imara wa ukuaji wa uchumi na muarobaini wa tatizo la ajira kwa sababu vinaajiri watu wengi wenye kada za aina mbalimbali. Pia amewataka vijana kujishughulisha na shughuli mbalimbali zitakazowapatia kipato cha halali na wasubiri kuajiriwa tu.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa soko la Holili wilayani Rombo, Septemba 7, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Aliyasema hayo jana jioni ya Septemba 7, 2020 alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Polisi Tarakea wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wakati akimuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Rombo Profesa Adolf Mkenda na wagombea udiwani kupitia CCM.

 

Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Tano imehamasisha wawekezaji kujenga viwanda nchini lengo likiwa ni kukuza uchumi wa Taifa na wananchi kwa ujumla kwa sababu viwanda vinatoa ajira kwa watu wengi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, usafirishaji.

 

Alisema wananchi wanatakiwa kumchagua Rais Dkt. Magufuli ili aendelee kusimamia mikakati ya kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda ambayo aliianzisha. “Wanatarakea mnafahamu mambo makubwa aliyofanya Rais Dkt. Magufuli katika Taifa hili. Nawaomba siku ikifika tumpigie kura za kutosha.”

Wananchi wa Rombo wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa  na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati alipohutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Polisi Tarakea, Septemba 7, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Alisema Rais Dkt. Magufuli ameliletea heshima kubwa Taifa ndani na nje ya nchi kutokana na uhodari wake katika kufanyakazi ya kuwaletea maendeleo Watanzania wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, kidini wala kikabila, hivyo ni vema wakaonesha shukurani zao kwa kumchagua ili aendelee kuongoza.

 

Akizungumzia upatikanaji wa nishati ya umeme wilayani Rombo, Mheshimiwa Majaliwa alisema kati ya vijiji 519 vilivyopo Rombo vijiji vyenye umeme ni 498 na 21 havina. “Vijiji vyote visivyokuwa na umeme vitawekewa umeme kwani tayari mkandarasi yupo Rombo anaendelea na kazi.”

 

Alisema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Rombo. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.

 

Pia Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali yao.

 

MOSHI MJINI

 


Pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wajasiriamali wa aina mbalimbali nchini katika kujenga na kuboresha zaidi sekta binafsi itakayoshirikiana nayo katika kutoa mchango wenye manufaa makubwa kwa Taifa.

Mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM wa jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo  (kushoto) na mtia nia wa uteuzi wa CCM katika kugombea nafasi hiyo, Ibrahim Shayo wakiudhihirishia  umma kuwa wapo pamoja wakati Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipowakutanisha kwenye jukwaa kuu na kuwasihi wavunje ukimya. Ibrahim alitamka hadharani kuwa atamuunga mkono mgombea wa CCM Tarimo. Walikuwa katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Waziri Mkuu kwenye uwanja wa Majengo mjini Moshi, Septemba 6, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 imeielekeza Serikali ihakikisha katika kipindi cha miaka mitano ijayo, watendaji wake wanaendelea kuwa na mtazamo chanya juu ya sekta binafsi na kuishirikisha kikamilifu katika uwekezaji, hususani ujenzi wa viwanda kwa kuimarisha Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (Blue Print).

 

Aliyasema hayo juzi jioni ambapo ilikuwa Septemba 6, 2020 alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Majengo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akimuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo na wagombea udiwani.

 

Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kuandaa jukwaa maalumu kwa ajili ya kutangaza vivutio vya uwekezaji vilivyoko ndani ya mkoa huo ili kushawishi wawekezaji kwenda kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda.

 

Alisema,uwepo wa viwanda vingi utasababisha wananchi hususani vijana kupata ajira kwa sababu viwanda vinaajiri watu wengi wenye kada za aina mbalimbali. Pia amewataka vijana kujishughulisha na shughuli mbalimbali zitakazowapatia kipato cha halali na si kusubiri ajira za kutoka Serikalini pekee.

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kusimamia nidhamu kwa watumishi wa umma na kudhibiti vitendo vya rushwa ili wananchi wanufaike na kuifurahia nchi yao.

 

Alisema,jukumu kubwa la watumishi wa umma ni kuwatumikia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote, hivyo aliwataka waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu. Aliwaomba wakazi wa Moshi na Watanzania wawachague wagombea wa CCM ili maendeleo yaendelee kupatikana katika maeneo yao.

 

“Nimekuja hapa kumuombea kura Rais Dkt. Magufuli. Hakikisheni ifikapo Oktoba 28, 2020 mnapofika katika vituo vya kupigia kura unachukua karatasi ya kupigia kura na kumchagua Rais Dkt. Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano mingine. Mnafahamu vizuri kazi kubwa aliyoifanya miaka mitano iliyopita,"alisema.

 

Waziri Mkuu alisema kuwa, katika kipindi cha miaka mitano ya serikali ya Rais Dkt. Jonh Pombe Magufuli imeweza kuhakikisha inaboresha huduma za afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mkoa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora na kwa ukaribu.

 

Alizitaja baadhi ya huduma hizo ni pamoja na kuboresha usafiri wa treni na kupunguza gharama kwa wananchi ambapo kwa sasa treni ya abiria kutoka jijini Dar es Salaam hadi Moshi/ Arusha ipo mara nne kwa wiki kwa nauli ya sh. 6,000 tu tofauti na nauli ya basi ambayo ni sh. takribani 40,000. Aidha, usafirishji wa mizigo kwa mwezi umefikia wastani wa tani 1,500 hadi 2,500.

 

Pia, Waziri Mkuu alitumia mkutano huo kuwakutanisha mgombea ubunge wa CCM jimbo la Moshi Mjini, Tarimo na mtia nia aliyeomba uteuzi wa CCM katika jimbo hilo lakini hakuteuliwa, Ibrahim Shayo ambaye alitamka hadharani kuwa atamuunga mkono mwenzake Tarimo ili kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika jimbo hilo.

 

 

 

 

 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news