Mchungaji Peter Msigwa:Chagueni madiwani,wabunge na Rais kutoka CHADEMA, mwaka huu hakuna wasaliti

Mgombea wa Ubunge Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa amewahakikisha wapiga kura kuwa hakutakuwa na diwani wala mbunge au rais atakayekihama chama hicho kwa kuwa wameteua viongozi wanaokipenda chama hicho kuliko mwaka 2015, anaripoti Fredy Mgunda (Diramakini) Iringa.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika Kata ya Ruaha,Msigwa amesema kuwa, baadhi ya madiwani walihamia CCM kwa ajili ya uroho wa fedha na madaraka na walikuwa hawana nia njema ya kuwatumikia wananchi katika kata zao.

Msigwa amesema kuwa, wagombea wa udiwani katika uchaguzi wa mwaka huu wamewateua wagombea ambao ni viongozi kweli na wenye nia njema ya kuwatumikia wananchi katika kuwaletea maendeleo.
Mgombea Ubunge Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa akiwa kwenye mkutano wa kampeni Kata ya Ruaha mkoani Iringa. (Diramakini).
 
Msigwa aliwaomba wananchi wa Kata ya Ruaha kupigia kura mgombea wa ubunge, udiwani na urais wa CHADEMA kwa kuwa hao ndio viongozi bora katika uchaguzi wa mwaka huu.

Aliwakumbusha wananchi wa Kata ya Ruaha kukichagua Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) kwa kuwa ndio chama ambacho kimesaidia kuleta maendeleo yanayoonekana hivi sasa kwenye kata hiyo.
Baadhi wananchi waliojitokeza kumsikiliza Mgombea Ubunge Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa (hayupo pichani) akiomba kupewa ridhaa ya kuwa mbunge tena. (Diramakini).

Aidha Msigwa aliwaomba wananchi kuwapigia kura kwa wingi wagombea wa CHADEMA ngazi zote kwa kuwa chama hicho kimejipanga vilivyo kuzilinda kura za wananchi hao zisiibiwe na wapinzani wao.

Kwa upande wake mgombea wa udiwani Kata ya Ruaha kupitia cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Patrick Nyaulingo amesema kuwa, wananchi wanapaswa kuchagua wagombea wa CHADEMA kwa ajili ya kupata maendeleo ya uhakika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news