MGOMBEA Urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Bernard Membe amesema akichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Serikali atakayounda na kuongoza haitawabughuzi wafanyabiashara wadogo wanaonunua mazao kwa wakulima ambao katika mikoa ya Lindi na Mtwara wanatambulika kama kangomba.
Ametoa ahadi hiyo leo Septemba 1, 2020 wakati wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mpilipili Manispaa ya Lindi.
Uzinduzi ambao pia ulihudhuriwa na Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe na mwenyekiti wa taifa, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye pia ni mgombea urais kupitia chama hicho katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Amesema, anatambua kwamba nchi zote zilizofanikiwa kiuchumi duniani zinategemea wafanyabiashara wa kati, hivyo atawaruhusu wananunue mazao kwa wakulima bali walipe kodi sahihi.Membe amesema, hata wanaonunua mazao kwa wakulima kutoka mataifa ya nje ni kangomba wa kimataifa. Hivyo haoni sababu ya kuwaruhusu kangomba wa ndani kununua mazao ya wakulima. Bali kubwa ni kuhakikisha wanalipa kodi.
Pia amehaidi kupita katika mikoa yote kuzungumzia changamoto za kila mkoa ambazo wananchi wanakabiliana nazo ili kuwapa matumaini ya kutatua changamoto hizo iwapo atachaguliwa kuwa Rais.
Katika kuhakikisha azima yake hiyo inafanikiwa, Membe amejinasibu kwamba ataunda wizara ya biashara ambayo itakuwa na wajibu wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima."Wakulima watapeleka na kuuza mazao yao popote bila ya kuingiliwa na serikali, bali walipe kodi," amesisitiza Mgombea urais huyo.
Katika hatua nyingine Membe amesema anauhakika wakushinda uchaguzi. Kwani hata ndani ya Chama Cha Mapinduzi wapo wengi wanaomuunga mkono kutokana na kuchoshwa na hali ya mambo.
Membe amesema, kama atakuwa Rais atapandisha mishahara ya watumishi na kuwapandisha madaraja. Kwani ni haki ya watumishi wa umma. Huku akihaidi kuwalipa fedha za likizo.
Mgombea huyo licha ya kuhaidi hayo, lakini pia amehaidi kuimarisha ushirikiano na mataifa mbalimbali duniani. Kwa madai kwamba hivi sasa Tanzania imekuwa kama kisiwa kilichojitenga na mataifa mengine kuhusu mahusiano na ushirikiano.
"Nawafurahia sana wana CCM, kwani wamechoka, wananiunga mkono. Wapo wanaosema watabaki na kadi tu,"amesema Membe.