Mgombea Ubunge katika Jimbo la Musoma Mjini Kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Julius Mwita, amesema endapo atashinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu atahakikisha anaanzisha Dawati Maalumu la kusikiliza changamoto zinazoyakabili makundi maalumu ikiwemo wazee na walemavu,anaripoti Amos Lufungulo, Mara.
Wafuasi wa Chadema wakifuatilia mkutano wa kampeni wa Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Mjini, Julius Mwita uliofanyika Majitarod Musoma.(Diramakini).
Mwita amesema kuwa, makundi maalumu katika kata za Manispaa ya Musoma, yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ugumu wa maisha pamoja na huduma hafifu za matibabu, hivyo akichaguliwa dawati atakaloanzisha litakuwa mahususi kukusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi tofauti na Sasa.
"Tunao wazee ambao kimsingi wengine hawana msaada wowote wanaopewa, hata huduma zao za matibabu wakati mwingine ni ngumu kuzipata kwa wepesi, nikichaguliwa nitaanda dawati ambalo litaratibu changamoto zao na ikiwezekana litapita kata kwa kata kuwafuatilia wazee kusudi iwe rahisi kuwasaidia,"amesema.
Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Mjini kupitia (Chadema),Julius Mwita akizungumza katika Mkutano wa kampeni uliofanyika Majitarod Manispaa ya Musoma. (Diramakini).
Amesema pia, atashughulikia changamoto za wavuvi ambazo zimekuwa zikiwasibu mara kwa mara kusudi waweze kunufaika na rasilimali hiyo katika kuwakwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini, ambapo kwa sasa amesema mchango wa rasilimali hiyo hauwanufaishi wavuvi na wananchi kwa ujumla.
"Musoma tunao mwalo wa dagaa na samaki uliopo Makoko, nikichaguliwa nitahakikisha nawezesha uweze kujengwa uwe wa kisasa kusudi wafanyabiashara kutoka nchi za nje waje kununua samaki, dagaa, hatua hii itainua uchumi wa wavuvi, wafanyabiashara na uchumi wa Musoma Mjini,"amesema Mwita.
Asha Khamis na Pendo Juma Wakazi wa kata ya Mwisenge wakizungumza na Diramakini kwa nyakati tofauti baada ya mkutano huo kuahirishwa wamesema, watafurahi endapo ahadi ya kuboresha mwalo wa samaki wa Makoko ataitekeleza Mwita iwapo atashinda, kwani utakuza uchumi wa wafanyabiashara wa samaki na dagaa katika Manispaa ya Musoma.