Mgombea Ubunge Devota Minja kupitia CHADEMA aja na tumaini jipya la kurejesha viwanda

Mgombea ubunge Jimbo la Morogoro Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Devota Minja amesema kuwa akichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo atahakikisha viwanda vyote vilivyokufa vinafufuliwa, kwani vinategemewa na wanawake wengi kujipatia ajira kutoka ndani na nje ya mji huo.
Minja amesema kuwa, mkoa huo umebarikiwa kuwa na viwanda vingi, lakini havifanyi kazi kwa kuwa vilichukuliwa na watu wasiokuwa na uwezo wa kuviendesha.

“Mkoa wa Morogoro hususani Manispaa ya Morogoro kuna viwanda vingi ambavyo havizalishi, nikichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hili nitajitoa kuhakikisha viwanda hivyo vinafanya kazi ili akina mama wa Morogoro wapate ajira katika viwanda hivyo,”amesema.

Minja amesema kuwa, viwanda maeneo mengi nchini vimekuwa ni mkombozi wa ajira kwa wanawake kwani takwimu zinaonesha kuwa wanawake hupata ajira kwa wingi viwandani kuliko ofisini na hivyo kuwawezesha kujikimu kimaisha.

“Mfano kKwanda cha Tumbaku ambacho kwa sasa kimesimama uzalishaji kilikuwa kinaajiri watu 5,000, wengi wao wakiwa wanawake,Kwa hiyo viwanda vinajulikana duniani kote kuwa ndio ajira inayoeleweka kwa wanawake, sehemu pekee ya wanawake ambayo wanaweza wakapata hata kazi ya kupepeta, kufanya usafi, kufunga na mengineyo ni viwandani,"amesema Minja.

Ameongeza kuwa, maisha ya wakazi wa Morogoro yamekuwa magumu kwa kuwa wengi wao hawana ajira kutokana na viwanda vingi kufungwa.

“Mimi nitakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba tunafufua hivyo viwanda, kwa sababu vilijengwa kwa jasho na kodi za Watanzania, vilibinafsishwa vikiwa vinafanya kazi, lakini waliovimaliza na kuviua viwanda hivyo lazima tupambane nao, kama walishindwa kuviendeleza walitakiwa kuvirudisha serikalini,”amesema Minja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news