MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Ilemela jijini Mwanza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt.Angeline Mabula amesema kuwa ataendelea kuwatumikia wananchi wa Jimbo la
Ilemela kwa haki, usawa na uadilifu mkubwa kuhakikisha wananchi hao
wanapata maendeleo.
Dkt.Angeline Mabula ameyasema hayo wakati
akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho na wananchi katika mkutano
wa hadhara wa kampeni ya uchaguzi uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Masemele Kata ya Shibula.
Amesema katika kipindi hicho hospitali ya wilaya imejengwa, shule mpya tatu za msingi na sekondari zimejengwa, miradi mikubwa ya maji imejengwa na urasimishaji wa makazi na umilikishaji ukifanyika kikamilifu huku jimbo hilo likiongoza kwa zoezi hilo kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
"Yapo mambo mengi tumeyafanya kwa
kipindi cha miaka mitano iliyopita ambayo hayakuwepo. Niwaombe ndugu
zangu mtuchague tena mimi binafsi kuwa mbunge wenu, Mheshimiwa Rais Magufuli na
madiwani ili tukatekeleze shughuli za maendeleo kutoka pale tulipoishia,"amesema.
Mgombea Ubunge huyo ameahidi kuendeleza
michezo kwa wananchi hao kupitia mashindano aliyokuwa akiyaendesha ndani
ya jimbo hilo yanayojulikana kama ‘The Angeline Ilemela Jimbo Cup’ huku akiwasisitiza kutouza viwanja kiholela na kutokacha zoezi la umilikishaji kwa faida yao binafsi na vizazi vyao.
Akimkaribisha
mgombea ubunge huyo, Meneja Kampeni wa Jimbo la Ilemela, Ndugu Kazungu
Safari Idebe amewataka wananchi hao kuwapuuza wanasiasa wasiokuwa na nia
njema wanaohubiri chuki, utengano na kukwamisha maendeleo kwani CCM
kupitia mgombea wake wa urais, Dkt John Magufuli na Serikali yake
wametekeleza shughuli kubwa ya kuwaletea watanzania maendeleo ikiwemo
ukamilishaji wa miradi ya reli ya kisasa, mradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, ununuzi wa ndege, ujenzi wa hospitali, zahanati na vituo vya
afya.
Wakati Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Ilemela, Nelson Mesha akiwaomba wananchi hao kukiunga mkono chama chake na
wagombea wake kwani wamebeba Ilani yenye dira na maono ya Tanzania
wanayoitaka.
Kampeni za mgombea Ubunge wa Jimbo la Ilemela
kupitia CCM zitaendelea tena leo katika Kata ya Kitangiri,viwanja vya Mihama jimboni humo.