MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO KUUNGANISHA VISIWA VYA PEMBA NA UNGUJA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeweka saini ya mkataba wa makubaliano wa kuunganisha visiwa vya Pemba na Unguja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa Zanzibar,anaripoti Prisca Ulomi, WUUM, Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri Kindamba akiongea na waandishi wa habari kabla ya kutia saini mkataba wa makubaliano wa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na visiwa vya Pemba na Unguja wakiwa kwenye ukumbi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Zanzibar. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Mustafa Aboud Jumbe na Dkt. Zainabu Chaula (wa pili kushoto) wa Wizara hiyo (Sekta ya Mawasiliano), Tanzania Bara.(WUUM).

Utiaji saini huo umeshuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Mustafa Aboud Jumbe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kabla ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa makubaliano wa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na visiwa vya Unguja na Pemba wakiwa kwenye ukumbi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Zanzibar. Kushoto ni Katibu wa Wizara hiyo, Dkt.Mustafa Aboud Jumbe.(WUUM).

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri Kindamba (kulia), akipeana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA Zanzibar, Mhandisi Shukuru Suleiman baada ya kusaini mkataba wa makubaliano wa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na visiwa vya Unguja na Pemba wakiwa kwenye ukumbi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na usafirishaji, Zanzibar.(WUUM).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Dkt.Mustafa Aboud Jumbe akiwa ofisini kwake akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) wa Tanzania Bara, Dkt. Zainabu Chaula kabla hawajashuhudia utiaji saini wa mkataba wa makubaliano wa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na visiwa vya Unguja na Pemba.(WUUM).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula (wa pili kulia) akiwa ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar (wa pili kushoto), Dkt. Mustafa Aboud Jumbe kabla ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa makubaliano wa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na visiwa vya Pemba na Unguja. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri kindamba akisikiliza. (WUUM).

Utiaji saini huo umefanywa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba kwa upande wa Bara na Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA Zanzibar (ZICTIA) kwa upande wa Zanzibar

Kabla ya kushudia tukio hilo, Dkt. Zainabu Chaula alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 700 na kuunganisha kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kwenye nchi jirani za Congo, Zambia, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Malawi ambapo maunganisho haya yanaenda kufungua fursa za wawekezaji na watumia wa huduma za mawasiliano wa ndani na nje ya nchi kuunganishwa na Zanzibar kwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano tumeshuhudia kuibuka kwa mifumo ya TEHAMA ambayo inawezesha utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi kwa kasi zaidi.

Naye Dkt. Jumbe amesema kuwa haya ndio matunda ya mapinduzi, matunda ya mapinduzi sio maembe wala mapapai bali ni maendeleo yanayopatikana katika nchi yetu, na Serikali yetu ya SMZ imetumia zaidi ya shilingi bilioni 30 kuunganisha mikoa na wilaya zote za Unguja na Pemba bali kulikuwa na changamoto ya kuunganisha Unguja na Pemba ila sasa kwa kupitia makubaliano haya, tutatumia barabara ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuunganisha visiwa Pemba na Unguja na hivyo Zanzibar kuunganishwa na Tanzania Bara moja kwa moja na utawezesha kupunguza gharama za mawasiliano ili ziwe nafuu

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa miundombinu ya TEHAMA, Zanzibar, Mhandisi Shukuru Suleiman akiongea na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Zanzibar kabla ya kusaini mkataba wa makubaliano wa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na visiwa vya Pemba na Unguja. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Mustafa Aboud Jumbe, wa pili kushoto ni Dkt. Zainabu Chaula wa Wizara hiyo (Sekta ya Mawasiliano), Tanzania Bara na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri kindamba wa kwanza kulia akisikiliza.(WUUM).

Ndugu Kindamba amesema kuwa, ufunguzi wa njia za mawasiliano ya Mkongo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar utakuwa na manufaa makubwa sana kwa taifa hasa katika kuwezesha kuongezeka kwa matumizi ya data na intaneti na makubaliano hayo yanahusisha kutunza vifaa vya miundombinu ya TEHAMA vya ZICTIA kwenye majengo ya TTCL.

Mhandisi Suleimani ameongeza kuwa, ZICTIA imekamilisha ujenzi wa Mkongo wa Zanzibar na sasa unaunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambapo itakuza na kuongeza huduma za mawasiliano; kuondoa changamoto iliyokuwepo Zanzibar ya kutumia njia ya mawasiliano ya mawimbi ya radio kutoa huduma za mawasiliano ambayo hayana kasi na ubora unaohitajika, kupunguza gharama za mawasiliano na kuingizia mapato kwa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news