Burudani hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, ilikuwa na lengo la kumpongeza Dkt.Hussein Mwinyi kwa kuteuliwa kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar kutoka CCM.
Katika taarabu hiyo nyimbo mbalimbali mpya na za zamani ziliimbwa na kuwafanya wapenzi wa muziki huo wa taarabu asilia kushindwa kujizuia kwenye viti vyao muda wote.
Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na ile ya ‘pongezi kwa mgombea’ iliyoghaniwa kwa umahiri mkubwa na al-anisa Fatuma Dawa.
Nyingine ni ‘Mpewa hapokonyeki’ (al-anisa Mtumwa Mbarouk), ‘hongera Dkt. Shein (ustadh Idd Suweid),’wahoi (al-anisa Sabina Hassan) pamoja na ‘Tunapendana iliyoghaniwa na mwimbaji maarufu al-anisa Fatma Abdisalami.
Aidha, nyimbo nyingine ambazo ziliwafanya wasikilizaji kutabasamu na kuibua shangwe na nderemo ilikuwa ni pamoja na ‘Zanzibar ya Dkt.Hussein Mwinyi’ iliyoimbwa na al-anisa Mgeni Khamis, ‘Haya maumbile yangu (al-anisa Amina Abdalla), ‘kama kupenda ni dhara (ustadh Idd Suweid) pamoja na ‘Mazoweya yana taabu iliyoghaniwa na al-anisa Fatma Dawa.
Katika hatua nyingine, mgombea wa Urais wa Zanzibar kutoka CCM, Dkt.Hussein Mwinyi alitumia fursa hiyo kuzungumza na washiriki wa burudani hiyo na kutoa shukurani za dhati kwa Dkt.Shein kwa kuandaa burudani hiyo iliyofana.
Alisema, kwa kipindi chote tangu alipoteuliwa na chama hicho kuwa mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar mjini Dodoma, ameendelea kupata ushirikiano mkubwa na wanachama wa chama hicho, chini ya uongozi wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.
Aidha, ameelezea kuridhishwa kwake na maandalizi ya kampeni yanayoendelea kufanyika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.
Dkt. Mwinyi aliahidi kuyaendeleza mambo yote mazuri yaliosisiwa na mtangulizi wake pamoja na kuweka ahadi ya kufanyika burudani ya aina yake baada ya chama hicho kufanikisha azma yake na kuingia Ikulu.
Hafla hiyo iliyoandaliwa na Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar pia iliwashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Ali Idd pamoja na mke wa mgombea Urais wa Zanzibar Mwinyi.