Daktari Alex Kanjanja akimsikiliza mwananchi aliyefika katika banda la NHIF katika maonyesho ya dhahabu mjini Geita ili kupata huduma mbalimbali za kitabibu.(Diramakini). |
Meneja wa NHIF Mkoa wa Geita, Elius Odhiambo amesema leo Septemba 22, 2020 kuwa, mwelekeo wa mfuko ni kumfikia kila mtu kupitia makundi mbalimbali kama vile watumishi wa umma na wafanyakazi wa taasisi au mashirika binafsi.
Odhiambo amesema hayo katika Maonesho ya Teknolojia ya Dhahabu yanayofanyika mjini Geita ambapo mfuko huo unaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
Meneja Odhiambo ametaja makundi mengine kuwa ni pamoja na machinga,waandishi wa habari kupitia klabu zao,vikundi vya wajasiriamali,bodaboda,machinga,Saccos na wachimbaji wadogo wadogo.
Meneja huyo ameongeza kuwa, kupitia makundi hayo mfuko huo utaweza kumfikia kila mwananchi na kujiunga katika mfuko na kunufaka na huuma zake.
Amewataka wananchi mkoani Geita kujenga tabia ya kujitokeza kupima afya zao mara kwa mara ili kuweza kubaini magonjwa mbalimbali yanayoweza kutibiwa mapema ili kulinda afya zao na kutibika kwa urahisi na kwa gharama nafuu hasa magonjwa yasiyoambukizwa kama shinikizo la damu,kisukari na uwiano na uzito wa mwili ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
Odhiambo amesema kuwa, katika maonyesho hayo wana wataalamu wa afya ambao wako tayari kuhudumia watu wote watakaofika kwenye banda lao.
Amesema, katika maonyesho hayo NHIF ina majukumu matatu ambayo ni kutoa elimu ya umuhimu wa kuwa na bima ya afya,kuandikisha wanachama wapya katika mfuko ambao ni waajiriwa,watoto chini ya miaka 18 kupitia mpango maalum wa bima ya afya kwa watoto.
Aidha, amesema kuwa kazi nyingine inayofanywa na NHIF katika maonyesho hayo ni pamoja na kupima magonjwa mbalimbali ambayo siyo ya kuambukizwa kama vile shinikizo la damu,macho,uwiano wa urefu na uzito pamoja na kisukari.Vipimo hivyo vyote vinatolewa bure kwa kila mwananchi anayetembelea banda hilo na kuwa tayari kupima.
Dkt.Alex Kanjanja amesema kuwa, wanatoa huduma ya kupima magonjwa
yasiyoambukiza kama shinikizo la damu,kisukari na uwiano wa urefu na
uzito kwa kila mwananchi anayefika katika banda hilo.
Ameongeza kuwa,watu wengi wanaopima kisukari wanajikuta wako kwenye hatari ya kuugua au tayari wanaumwa, lakini wanakuwa hawajitambui kama wana magonjwa hayo.
Maonyesho hayo yalianza Septemba 17, mwaka huu na yanatarajiwa kuhitimishwa Septemba 27, mwaka huu amabayo yamekutanisha makampuni,taasisi na wajasiriamali wapatao 420.
Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa yenye migodi mingi ya uchimbaji madini hususani dhahabu ambapo shughuli hizo zinahusisha kutimuliwa vumbi wakati wa uchimbaji wa madini ambapo kwa taratibu za kiafya kila anayeshiriki shughuli hizo anatakiwa kuwa na vifaa vya usafi kwa ajili ya kujikinga.
Maonyesho ya dhahabu yanafanyika katika Kijiji Maalum cha Maonyesho Mtaa wa Bombambili Mjini Geita ambayo yanafanyika kwa mara ya kwa mwaka wa tatu mfululizo mkoani hapa.
Maonyesho hayo kwa mara ya kwanza yalifanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala mjini Geita kwa awamu mbili kwa kuratibiwa na Mamlaka ya Biashara nchini (TanTrade) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Malengo ya maonyesho hayo ni kuwaleta pamoja wachimbaji wa madini ili kubadilishana uzoefu na teknolojia katika sekta hiyo.