OPERESHENI ZA TAKUKURU MKOANI SINGIDA ZAOKOA MILIONI 199,559,254/= IKIWEMO MIKOPO UMIZA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imefanikiwa kuokoa kiasi cha sh. 199,559,254 kufuatia operesheni mbalimbali zilizofanywa ili kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa mkoani humo katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2020, anaripoti MARY MWAKAPENDA kutoka MANYONI.
 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni mstaafu, George Mkuchika aliyasema hayo jana wakati akimkaribisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika akitoa maelezo kuhusu jengo la TAKUKURU Wilaya ya Manyoni kabla ya kumkaribisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Job Ndugai kuzungumza na wananchi na kulizindua jengo hilo.

Mkuchika aliyataja baadhi ya maeneo ambayo operesheni hiyo iliyalenga kuwa ni pamoja na mikopo umiza ambapo kiasi cha sh. 58,150,000 kiliokolewa, kwa upande wa mapato yatokanayo na usimamizi wa madini, kiasi cha sh. 44,623,254 kiliokolewa, sanjari na hayo, kiliokolewa kiasi cha sh. 11,456,500 kutokana na mapato ya usimamizi wa minada, na kiasi cha sh. 85,329,500 kilirudishwa kutoka kwa wanachama wa vyama vya ushirika.

Waziri Mkuchika alifafanua kuwa, jitihahada zote hizi zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na TAKUKURU zinatokana na weledi, ujasiri na uzalendo uliopo katika kushughulikia tatizo la rushwa nchini, hivyo ameitaka TAKUKURU kuendelea na kasi hiyo ili kudhibiti vitendo vya rushwa na ufisadi nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika akimkaribisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Job Ndugai kuzungumza na wananchi kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida jana.

Katika eneo la utoaji elimu dhidi ya vitendo vya rushwa, Mkuchika aliainisha kuwa, TAKUKURU imefanikiwa kufungua na kuimarisha klabu 234 za Wapinga Rushwa shuleni na vyuoni na kutoa semina pamoja na mikutano ya hadhara 225.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai (kushoto) akisoma kibao cha ufunguzi wa jengo baada ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida jana. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Bibi Rahabu Magwisa.

Aidha,Mkuchika alimuahidi Spika Ndugai kujenga Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kongwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa tarehe 22 Julai, 2020 wakati akifungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chamwino na kuongeza kuwa, hatua hii inadhirisha nia ya dhati ya Serikali ya kupambana na vitendo vya rushwa nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika akiipongeza Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Sekondari ya Mlewa Wilayani Manyoni wakati wakiimba wimbo wa mapambano dhidi ya rushwa kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Manyoni mkoani Singida jana. 
 
Jengo la Ofisi ya TAKUKURU la Wilaya ya Manyoni ni mojawapo ya majengo saba ambayo Rais Magufuli alitakiwa kuyafungua kwa pamoja tarehe 22 Julai, 2020 wakati akifungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chamwino, Dodoma. Hata hivyo, aliweka utaratibu wa kuyafungua kwa nyakati tofauti na kumuelekeza Ndugai kulifungua jengo hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news