Profesa Muhongo: Neema ya mafanikio ipo CCM, msikubali kurubuniwa, baada ya Oktoba nitaanza kutekeleza haya

MGOMBEA Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo ameendelea na kampeni za kunadi sera na kuomba kura kwa wananchi wa Kijiji cha Kataryo Kata ya Tegeruka.

 Amesema, endapo atachaguliwa atahakikisha kwa kipindi cha miaka mitano anawezesha ujenzi wa chuo cha ufundi (VETA) kitakachotoa mafunzo ya  fani mbalimbali ikiwemo madini ili kutatua tatizo la ajira kwa vijana wanaohitimu kidato cha nne, cha sita,  vyuo vya kati na vyuo vikuu, anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.

Mbali na hilo, amesema amedhamiria kuendelea  kuimarisha mazingira bora ya wachimbaji wadogo wadogo katika Mgodi wa Kataryo ambapo atahakikisha pia sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi zinakua kwa kasi kubwa ili kuimarisha uchumi wa wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini pamoja na kusimamia kwa karibu sana uwezeshaji wa mikopo bila riba kwa kinamama, vijana na walemavu, ambapo vikundi 70 vilivyopo, kipindi hiki vilipewa shilingi milioni 350.
Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Vijini, Prof. Muhongo akizungumza katika mkutano wa kampeni Kijiji cha Kataryo Kata ya Tegeruka.(Amos Lufungilo/Diramakini).
Prof. Muhongo amewaondolea wasiwasi kuhusu upatikanaji wa  huduma ya maji safi na salama kutokana na mradi mkubwa wa maji wa Abadea  utakaotekelezwa kwa gharama ya shilingi  Bilioni 70 ambao utaanza kutekelezwa na Serikaki, na  hivyo maji yatakuwa ya uhakika  katika vijiji vyote vya kata ya  Mugango, Tegeruka, na  maeneno mengine kwa hiyo tatizo la maji litaisha kabisa jimboni humo.

Kuhusu suala la elimu, Prof. Muhongo amesema andapo atachaguliwa ataendelea kushirikiana na wananchi, madiwani wa  CCM watakaochaguliwa kujenga vyumba vya madarasa  katika shule ambazo bado zinachangamoto hiyo, ambapo ametolea mfano kwa  kipindi kilichopita jumla ya vyumba vya madarasa  400 vimejengwa chini ya usimamizi wake,  huku akiongeza kuwa, kwa sasa jumla ya Sekondari tano mpya zinajengwa na hivyo ameahidi pia kuwezesha ujenzi wa maabara na nyumba za waalimu katika Kata ya Tegeruka. 

"Naomba tumchague Rais Magufuli katika Uchaguzi mkuu huu, madiwani wa CCM, na mimi Mbunge wa chama cha mapinduzi,  ili tutekeleze Ilani kwa ufanisi, hatuwezi  kumchagua diwani wa upinzani ana ilani yake aweze kuendana na kasi yetu ya maendeleo, Rais alipokuja Musoma kipindi hiki  nilimuomba lami na amekubali kuijenga cha msingi tumchague kwa kishindo ili atekeleze mambo haya mazuri kwa manufaa yetu sote, hivyo  Oktoba 28 tuchagueni  kwani neema ya mafanikio ipo CCM," amesema Prof.Muhongo. 

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Vijijini, Bwire Nyabukika amesema kuwa, chama cha mapinduzi ndicho chama pekee chenye uwezo wa kuendelea kuwaletea maendeleo thabiti Watanzania  na hivyo amewaomba Wananchi wa kata ya Tegeruka na Jimbo la Musoma Vijijini kiujumla kukichagua kuanzia ngazi ya chini  udiwani, hadi ya Taifa.

Neema Elias na Mwajuma Mafuru Wakazi wa kata ya Tegeruka  wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema. hawana shaka na uchapakazi wa Prof. Muhongo kwani kwa kipindi Cha miaka mitano mambo mengi ya Maendeleo amewezesha kufanyika ikiwemo kujenga Zahanati, vyoo mashuleni, na vyumba vya madarasa jimboni humo  kwa kushirikiana na wananchi wake, pamoja na kutumia fedha zake kwa ajili yao.

"Prof. Muhongo ameweza kuinua pia kwa kiwango kikubwa Uchumi wa Wananchi mfano, aligawa mbegu za alzeti na mihogo bure kwa wananchi tukalima, bado pia amekuwa akigawa majembe ya kisasa ya plau kwa vikundi mbalimbali lengo lake ni kuona  Wananchi tunainuka kiuchumi tukimpa miaka mingine mitano atafanya makubwa mengi kwa ajili yetu,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news