Serikali yadhamiria kupanua wigo wa kilimo cha umwagiliaji hadi hekta milioni moja

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imedhamiria kupanua wigo wa kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 694,715 za sasa hadi kufikia hekta 1,000,000 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kaimu Mkurugenzi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Daudi Kaali akimkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya wakati wa kikao kazi baina ya Katibu Kusaya, Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wahandisi wa mikoa kilichofanyika mjini Morogoro hivi karibuni. (Tume ya Taifa ya Umwagiliaji).

Akifungua kikao kazi cha siku mbili baina yake, Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wahandisi wa Umwagiliaji wa mikoa yote nchini mjini Morogoro, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amesema, Serikali imeamua kutilia mkazo kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo,uhakika wa chakula,kuinua kipato cha wakulima na kuongeza tija katika pato la taifa, anaripoti Aaron Mrikaria (Tume ya Taifa ya Umwagiliaji) Morogoro.

“Serikali imeweka malengo tuhakikishe kuwa ifikapo mwaka 2025 tunaongeza wigo wa miundombinu ya umwagiliaji kufikia hekta 1,000,000. Maagizo haya ya serikali hakika tutayatekeleza kwa nguvu zote, bidii, na weledi mkubwa na tunahakika tutafanikiwa kwa kuwa tuna raslimali watu na fedha za kutosha kutekeleza miradi ya miundombinu ya umwagiliaji,”amesema.

Baadhi ya watendaji wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wahandisi wa mikoa wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika mjini Morogoro hivi karibuni.(Tume ya Taifa ya Umwagiliaji). 

Kusaya ameongeza kuwa, nchi itakapokuwa na eneo kubwa la umwagiliaji ndipo tutakapojihakikishia usalama wa chakula, lakini pia tutajihakikishia upatikanaji wa tija katika suala la mazao ya chakula na yale ya biashara kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo.

Hivyo, Tanzania haitakuwa na upungufu wa chakula na badala yake itauza nje mazao mengi ya biashara na mengine yatatumika kama malighafi katika viwanda vyetu hapa nchini.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Daudi Kaali amesema, Tanzania ina eneo la hekta milioni 29,000,000 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji pamoja na vyanzo vingi vya maji yakiwemo mabwawa, mito, maziwa na maji chini ya ardhi, kwa hiyo kuna fursa kubwa ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.

Tume ya Umwagiliaji imejipanga kutekeleza miradi ya kimkakati katika mabonde yaliyoainishwa kama vile Bonde la Mto Rufiji na Bonde la Mto Ruhuhu na mengine mengi
Picha ya pamoja,wajumbe katika kikao kazi baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wahandisi wa mikoa. Waliokaa mstari wa mbele katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw.Gerald Kusaya, waliokaa wa pili kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliji, Bw. Daudi Kaali, waliokaa wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bi.Mary Mwangisa na waliokaa wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Mipango, Bw.Reginald Diymet, waliokaa wa pili kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Mipango wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Anna Mwangamilo. Waliosimama nyuma ni wahandisi wa mikoa. (Tume ya Taifa ya Umwagiliaji).

“Haya tumepanga kuyatekeleza, lakini utekelezaji wake unahitaji fedha kwa hiyo mkakati wa serikali ni matumizi ya shilingi Bilioni 986.5 zinazotarajiwa kutumika katika ujenzi wa sekta ya umwagiliaji na kati ya hizo serikali imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 80 na fedha nyingine zitatoka vyanzo mbalimbali ikiwemo ushiriki wa sekta binafsi.

"Hata hivyo tume imepanga kuanzisha tozo mbalimbali katika miradi ya kilimo cha umwagilisaji ili kugharamia maendeleo ya sekta ya umwagiliaji,"amesema.

Kaali ameongeza kuwa, kwa sasa nchi inahitaji malighafi nyingi za kilimo kutokana na ujenzi mkubwa wa viwanda hivyo ni vema sekta ya umwagiliaji ipewe msukumo ili ifikapo mwaka 2025 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iweze kutimiza malengo ya serikali kufikia hekta 1,000,000 za umwagiliaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news