MKUU wa Wilaya ya Kaskazin B, Rajab Ali Rajab ameifunga skuli ya maandalizi ya Amish Marafiki Kiwengwa kwa muda wa wiki moja ili kulitafutia ufumbuzi tatizo la mgogoro ulipo kati ya walimu pamoja na uongozi wa skuli hiyo.
DC Rajab amesema, ameamua kuifunga skuli hiyo kwa muda baada ya kubaini kuwepo kwa matatizo ikiwemo utaratibu wa uajiri wa walimu ambao wamekuwa wakiajiriwa bila ya kuingia mikataba ya kazi pamoja na skuli hiyo kushindwa kufuata taratibu za uanzishaji wa skuli za maandalizi zilizowekwa na Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Amesema kuwa, endapo sheria na taratibu zitazingatiwa zitasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi bila usumbufu.
Pia amesema, kwa mujibu wa sheria za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ni jukumu la kila
skuli kuanzisha kamati ya skuli ili iweze kushirikiana na uongozi wa
skuli pindi yanapotokea matatizo kama hayo.
Hata hivyo, DC Rajab amemuagiza Sheha wa Shehiya ya Kiwengwa kumtaarifu mmiliki wa skuli hiyo ndugu Rozana kufika ofsini kwake Mahonda pamoja na walimu hao ili waweze kulizungumza tatizo hilo kwa kina na kulitafutia ufumbuzi ili kila mtu apate haki yake.
Skuli ya maandalizi Amish Marafiki Kiwengwa ni skuli ya binafsi iliyoanzishwa na Mwekezaji Rozana mwaka 2019 jijini Zanzibar.