KAMPUNI ya Simu za Mkononi ya Airtel Tanzania Plc, imeilipa Serikali ya
Tanzania, shilingi 32.9 bilionI kama gawio na mchango maalum wa
maendeleo baada ya kupata faida katika Mwaka wa Fedha 2019/20,anaripoti
FARIDA RAMADHANI.
Mfano wa hundi mbili za fedha hizo
ziliwasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Airtel Tanzania
Plc, Bw. Gabriel Malata na kupokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango ambaye pia ndiye mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James
jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James (katikati) akipokea Hundi ya Mfano ya shilingi bilioni 18.99, kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Airtel-Tanzania,Gabriel Malata, ambayo ni sehemu ya shilingi bilioni 32.9 ambazo Airtel imeilipa Serikali ikiwa ni gawio na michango ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Wanaoshuhudia kuanzia kulia ni Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbutuka, Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano, Dkt. Zainabu Chaula na Mkurugenzi Mtendaji Airtel Tanzania, Bw. George Mathen (kushoto).
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, akizungumza wakati wa halfa ya kupokea gawio na michango kutoka Kampuni ya Airtel Tanzania, ambapo Serikali imepokea kiasi cha sh. bilioni 32.99 jijini Dodoma, zikiwemo shilingi bilioni 18.99 za gawio na shilingi bilioni 14 za michango ya maendeleo, hafla ya makabidhiano imefanyika jijini Dodoma.
Akikadidhi hundi hiyo, Bw. Malata amesema katika kiwango hicho cha
shilingi bilioni 32.99, shilingi bilioni 18.99 ni gawio na shilingi
bilioni 14 ni mchango maalum wa maendeleo kwa Serikali baada ya Kampuni
hiyo kupata faida ya bilioni 38.5 kwa mwaka unaoishia Desemba 2019/2020.
Akielezea mafanikio yaliyosababisha kampuni yake kutoa gawio
nono na michango ya maendeleo ya shilingi bilioni 1 kila mwezi, Bw.
Gabriel Malata alisema licha ya uwekezaji mzuri katika upanuzi wa
mtandao, idadi ya wateja imeongezeka kutoka milioni 11.4 Machi 2019
mpaka 13.3 milioni Machi 2020 na kwa sasa umiliki wa soko ni asilimia 27
kwa taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Airtel Tanzania, Bw. Gabriel Malata, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi gawio na michango ya maendeleo kwa Serikali jijini Dodoma. Serikali inamiliki asilimia 49 ya hisa katika kampuni hiyo na Kampuni ya Bharti Airtel inamiliki asilimia 51.
Ameongeza kuwa, Airtel Tanzania Plc imetoa ajira za moja kwa moja zaidi
ya 500 huku wanafanyakazi wa kigeni wakiwa saba tu na kupitia kampuni
hiyo, Watanzania 350,000 wamejiajiri kwa kuuza huduma za kampuni ya
Airtel Tanzania Plc kama vile kuuza vocha, mawakala wa Airtel Money
hivyo kuchangia maendeleo ya uchumi kwa kulipa ushuru kwa Serikali
Na
kwa kuunga mkono maendeleo ya serikali kama elimu na afya, Airtel pia
imetoa 2.3 bilioni kwenye ujenzi wa Hosptili mkoani Dodoma na kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (VETA) kuzindua elimu kwa
mtandao kupitia applikesheni ya VSOMO ambapo wanafunzi zaidi ya 500
wamehitimu. Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (wa kwanza kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Kampuni ya Airtel Tanzania Bi. Beatrice Singano akifafanua jambo baada ya kampuni hiyo kutoa gawio na michango ya maendeleo kwa Serikali yenye thamani ya shilingi bilioni 32.99. Kuanzia kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Bw. George Mathen, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Airtel Bw. Gabriel Malata na wa tatu kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango Benny Mwaipaja, katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango,
Bw. Doto James amesema tukio hilo la Kampuni ya Simu za Mkononi ya
Airtel kutoa gawio na mchango wa maendeleo wa shilingi bilioni 32.99 ni
la kihistoria baada ya Serikali na Kampuni hiyo kuingia makubaliano
maalumu ya kiutendaji na kiumiliki yaliyofanyika mwaka 2019.
“Baada
ya majadiliano makali nay a muda mrefu, hatimaye Kampuni ya Bharti
Airtel ilikubali kuongeza hisa za Serikali kutoka asilimia 40 hadi
asilimia 49 na Bartel imebakiwa na asilimia 51,” amefafanua Bw. James.
Ameipongeza
Kampuni ya Airtel Tanzania kwa kutoa kiasi hicho kikubwa cha gawio cha
cha shilingi bilioni 18.99 na kiasi kingine cha shilingi bilioni 14
zinazotokana na mchango wa kampuni hiyo kwa Serikali ambapo inatoa
shilingi bilioni 1 kila mwezi kuanzia mwaka jana na itakuwa ikifanya
hivyo katika kipindi cha miaka mitano ambapo jumla ya shilingi bilioni
60 zinatarajiwa kupatikana.
Bw. James alizitaka Kampuni na
Mashirika ambayo Serikali inamiliki hisa kuiga mfano wa Kampuni ya
Airtel ili fedha zinazopatikana zichangie shughuli mbalimbali za
maendeleo ya nchi ikiwemo kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo,
kuboresha huduma za jamii kama vile afya, elimu na maji kwa Watanzania
wote.
Meza kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara hiyo baada ya Serikali kupokea gawio na michango ya maendeleo yenye thamani ya sh. bilioni 32.99 kutoka Kampuni ya Airtel Tanzania jijini Dodoma.
“Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo bado zinatoa gawio dogo na zile ambazo hazitoi gawio, zinatakiwa kujitathmini na kuhakikisha zinafanya vizuri na kulipa gawio ili kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo,"amesisitiza Bw. James
Naye Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka amesema ofisi yake imeendelea kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha taasisi, mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa zinaendeshwa kwa tija na zinaendelea kutoa gawio endelevu kwa Serikali.
Awali, Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka aliipongeza Airtel Tanzania Plc kwa gawio na mchango wake wa maendeleo na kuitaka kuendelea kudhibiti matumizi na kuimarisha teknolojia katika utoaji wa huduma.
Aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni zote ambazo Serikali ni mwanahisa na kwamba wasiridhike na gawio walilotia bali mwakani watoe kiwango kikubwa zaidi kwa maendeleo ya nchi.