Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge leo Septemba 22, 2020 amefanya kikao kazi na mamia ya walimu wa shule za msingi zilizopo Wilaya ya Ilala kwa lengo la kujadili changamoto zinazowakabili na kuangalia namna bora ya kuendelea kuboresha hali ya elimu ambapo amewahakikishia walimu kuwa Serikali inaendelea kulipa malimbikizo yote wanayodai.
RC Kunenge amesema, baada ya kikao na walimu wa Ilala pia amepanga kukutana na walimu wa wilaya nyingine za mkoa huo ili aweze kuzipatia majibu changamoto zinazowakabili ambapo amewapongeza walimu wote wa mkoa huo kwa kazi nzuri wanayoifanya jambo linalofanya mkoa huo kuwa kinara wa ufaulu kila mara.
Aidha, RC Kunenge amemuelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala
kuwa, anapaswa kuhakikisha anatoa kipaumbele cha ajira kwa walimu ili
kuweza kukidhi changamoto ya uhaba wa walimu kwa baadhi ya shule.
Hata hivyo RC Kunenge ametoa wito kwa walimu na wananchi wa mkoa huo kuhudhuria mikutano ya kampeni za wagombea mbalimbali ili waweze kuchagua viongozi wenye kuleta maendeleo.