Shirika la Posta Tanzania, Benki ya Watu wa Zanzibar kutoa huduma za kifedha nchini

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mwinyi Talib Haji amepongeza Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kuanzisha ushirika wa kipekee unaohusisha taasisi mbili za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kuongeza wigo wa kuwahudumia wananchi katika huduma za kifedha. Dkt. Mwinyi ametoa pongezi hizo wakati akizindua huduma ya uwakala wa PBZ na PBZ katika ukumbi wa mikutano wa VETA uliopo jijini Dodoma, sanaripoti FARAJA MPINA (WUUM).
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe (aliyeketi kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Idd Haji Makame (aliyeketi kulia), wakitia saini Mkataba wa ushirika wa kutoa huduma za kifedha baina ya Shirika hilo na Benki ya PBZ. Aliyesimama nyuma mwenye tai ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mwinyi Talib Haji pamoja na baadhi ya watendaji wakishuhudia tukio hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa VETA, Dodoma.

Aidha, Dkt.Mwinyi ametoa rai kwa TPC na PBZ kuendelea kuaminiana kwa huduma wanazozitoa ili katika ushirika wao kila mmoja atumie huduma za mwenzie na kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, huku wakienda sambamba na ukuaji wa teknolojia na kuitumia ipasavyo katika kutimiza ndoto na malengo ya taasisi zao.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mwinyi Talib Haji akielekezana jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Kidawa Ahmed Saleh kabla ya kuzindua ushirika wa kutoa huduma ya fedha za benki hiyo kupitia Shirika la Posta Tanzania uliofanyika kwenye ukumbi wa VETA, Dodoma.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt.Jimmy Yonazi amesema TPC ni taasisi inayofanya vizuri chini ya Sekta ya Mawasiliano kwa kuwa wabunifu kujiendesha kibiashara, na kwa ushirika huu utaleta mwanga mpya kwa huduma za posta na huduma za fedha nchini na kuwa mfano kwa mataifa mengine ambapo ametoa rai kwa taasisi hizo kuhakikisha kuwa mataifa mengine ya Afrika yanajifunza kutoka kwao na kutumia ubunifu wa aina hii.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Mwinyi Talib Haji akitoa fedha kwenye dirisha la Shirika la Posta Tanzania katika uzinduzi wa huduma za uwakala baina ya Shirika hilo na Benki ya Watu wa Zanzibar uliofanyika kwenye ofisi za Posta mjini Dodoma.

 Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya PBZ, Idd Haji Makame, amesema kuwa utoaji wa huduma za PBZ kupitia Shirika la TPC utakuwa rahisi na nafuu kwasababu shirika la TPC lina mtandao mpana na linapatikana kila mahali nchi nzima huku kwa upande mwingine ushirika huu utaifanya PBZ ijulikane na kuwafikia wateja wengi zaidi.

Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la TPC, Hassan Mwang’ombe amesema kuwa ushirika huu wa uwakala wa PBZ ni mwendelezo wa Shirika lake la TPC katika kutimiza ndoto za kuwa kituo cha kutoa huduma mbalimbali mahali pamoja ili kuwawezesha wateja wa Shirika hilo na wananchi kupata huduma za aina mbali mbali mahali pamoja (one stop centre) ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma na waweze kuokoa muda wao badala ya kutafuta huduma kwenye ofisi au taasisi tofauti ambapo itawawezesha kuendelea na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.

Mwang’ombe amesema kuwa Shirika lake la TPC limeunganishwa na mashirika mengine ya posta yapatayo 660 ulimwenguni kote ambapo ushirika baina yao na PBZ utatoa fursa kwa wateja wao kutumia huduma za uwakala na huduma nyingine za TPC ndani na nje ya Tanzania
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Jimmy Yonazi akiteta jambo na PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe kabla ya uzinduzi wa huduma ya uwakala baina ya Benki ya Watu wa Zanzibar na Shirika hilo uliofanyika kwenye ukumbi wa VETA, Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Jimmy Yonazi akizungumza kabla ya uzinduzi wa huduma ya uwakala baina ya Shirika la Posta Tanzania na Benki ya Watu wa Zanzibar uliofanyika kwenye ukumbi wa VETA, Dodoma. Wanaomsikiliza wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Idd Haji Makame na anayefuata ni Hassan Mwang’ombe, PostaMasta Mkuu wa Shirika hilo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mwinyi Talib Haji (mwenye tai waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) baada ya kuzindua ushirika wao wa kutoa huduma ya fedha za benki hiyo kupitia Shirika hilo uliofanyika kwenye ukumbi wa VETA, Dodoma. kushoto waliokaa ni Postamasta Mkuu wa TPC, Hassan Mwang’ombe na kulia waliokaa ni Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Idd Haji Makame.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news