Soud na wenzake kizimbani kwa kukutwa na nyara za Serikali

ABDUL Soud, Failuna Matunda, Yusuph Rashid, Joseph Elio, Catherine Mayinda na Abdallah Mwinyo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kukutwa na silaha vikiwemo vipande vya meno ya tembo 24.Taarifa mpya soma hapa.

Meno hayo yanakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 240,054,948 kwa fedha za Kitanzania. Wakili wa Serikali, Candid Nasua akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate wa Mahakama hiyo amesema kuwa, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka naneWakili huyo amesema, katika shtaka la kwanza,washtakiwa wote kati ya Novemba 2019 na Agosti 2020 kwa pamoja waliunda genge la uhalifu na kujipatia vipande 24 vya meno ya tembo vyenye thamani hiyo mali ya Serikali ya bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Amedai kuwa, katika shtaka la pili la kukutwa na meno ya tembo linamkabili Sound, Matunda na Rashid, ambapo wanadaiwa Agosti 13, 2020 katika eneo la  Azimio wilayani Temeke jijini Dar es Salaam washitakiwa walikutwa na vipande hivyo kinyume cha sheria ya wanyamapori nchini Tanzania.

Wakili huyo alidai kuwa, katika kosa la tatu la kujihusisha na nyara za Serikali, washtakiwa wanatuhumiwa Agosti 13,2020 walishiriki kusafirisha vipande hivyo kinyume cha sheria.

Aidha, katika kosa la nne linalomhusu mshtakiwa Mayinda katika tarehe zisizofahamika na maeneo yasiyofahamika mshtakiwa huyo alighushi kadi ya mpiga kura yenye namba T-1004-2822-706-3 yenye jina la Bhoke M.Mwita ikionesha ni kadi halali kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi huku akijua si kweli.

Pia katika kosa la tano, Wakili huyo alidai kuwa Agosti 26, 2020 katika Kijiji cha Mtawanga wilayani Liwale Mkoa wa Lindi mshtakiwa Mwinyo alikutwa na silaha aina ya Riffle 458 kinyume cha sheria.

Shitaka la sita linamkabili mshtakiwa Soud, ambapo ilidaiwa Machi 5, 2020 alishindwa kuhifadhi silaha ipasavyo na kusababisha silaha hiyo kuangukia mikononi mwa mshtakiwa Mwinyo.

Aidha,shtaka la saba la kumiliki laini ya simu iliyokuwa ikimilikiwa na mtu mwingine, ilidaiwa kati ya Mei 1, 2020 na Agosti 24, 2020 mshtakiwa Mayinda alitumia laini ya simu iliyoonesha kumilikiwa na Joseph Elio ambaye naye alikabiliwa na shtaka la kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya umiliki wa laini ya simu kwa mtoa leseni.

Katika shtaka la mwisho la utakatishaji fedha ilidaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2018 na Agosti, 2020 katika maeneo tofauti mkoani Lindi na jijini Dar es Salaam washtakiwa wote walijipatia vipande hivyo vya meno ya tembo vyenye thamani hiyo ya fedha huku wakijua vipande hivyo vya meno ya tembo ni zao la kosa tangulizi la ujangili.

Hata hivyo, baada ya washtakiwa kumaliza kusomewa mashtaka hayo, Wakili Nasua alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ambapo kesi hiyo itatajwa Septemba 22,mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news