TAKUKURU yang'ata Mkurugenzi aliyeghushi nyara za TRA kujipatia zabuni

MKURUGENZI wa Kampuni ya JACO Service Group Company Ltd, John Steven Kabelinde (Babu Joha) ambaye ni mkazi wa Jiji la Dar es Salaam amefikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  kwa kuwasilisha nyaraka za upotoshaji na kujipatia zabuni. 
Akisoma Mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Manyara, Simon Kobelo, Mwendesha Mashtaka na Mwanasheria wa TAKUKURU,Eveline Onditi, ameeleza kuwa,mtuhumiwa anashtakiwa kwa kosa la jinai shtaka namba 153/2020.

Amesema, mshtakiwa anashtakiwa kwa makosa mawili ambapo kosa la kwanza ni la kughushi ambapo ni kinyume na kifungu cha 333, 335(a) na 337 cha sheria ya makosa ya jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Onditi ameeleza kuwa, Mkurugenzi na mmiliki wa kampuni ya JACO Service Group mnamo tarehe 13,2,2012 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa amenuia kufanya udanganyifu aliweza kuandaa hati ya uongo ya namba ya utambulisho ya mlipakodi TIN 101-325-695 ya tarehe 13,2,2002 ikionyesha kuwa Joha Steven Kabelinde amesajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwamba alipewa TIN namba 101-325-695 ambayo ilianza kufanya kazi 13,2,2020 suala ambalo  si kweli.

Mwendesha mashtaka huyo amesema katika shtaka la pili, mshtakiwa anashtakiwa kwa kosa la kuwasilisha nyaraka za uongo ambalo ni kosa kinyume na kifungu cha 342 cha sheria ya makosa ya jinai namba 16 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2019.

Inadaiwa kuwa John Steven Kabelinde akiwa ni Mkurugenzi mmiliki wa Kampuni ya JACO Service Group Company Ltd, kwa tarehe tofauti kati ya Julai 4,2019 na Septemba 11,2019 katika ofisi za Tanroads zilizopo wilayani Babati mkoani Manyara, huku akijua aliweza kufanya udanganyifu kwa kuwasilisha nyaraka yenye maelezo ya uongo ya TIN 101-325-695 ya tarehe 13,2,2002 ikionyesha ya kwamba TIN namba hiyo iliyokuwa imetolewa na Kamishna wa VAT wa TRA ikionyesha kwamba Bwana Joha Steven Kabelinde amekadiriwa kama mlipakodi ambapo TIN namba hiyo ilianza kutumika rasmi mnamo tarehe 13,2,2002.

Hata hivyo, mshtakiwa amekana mashtaka yote dhidi yake na shauri hilo litatajwa tena Septemba 17,2020.

Mshtakiwa yupo rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua yenye utambulisho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news