TAKUKURU yaokoa nyumba ya mama mjane

"Nimekutana nanyi leo hii ili tuzungumze kuhusu kazi ambayo TAKUKURU Mkoa wa Songwe imefanya ya kumsaidia mama mjane aliyekuwa anadaiwa nyumba yake aliyorithi kutoka kwa marehemu mume wake au kulipa fedha kiasi cha shilingi 40, 000,000 ambao ni mkopo umiza. Mama huyo mjane ilikuwa afukuzwe katika nyumba kutokana na mkopo huo;

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Songwe, Damas Suta ameyasema hayo leo mbele ya waandishi wa habari wakati akizungumzia juu ya hatua hizo.

 
Amesema, Septemba 2, 2020 mama mjane aitwaye Agness Mwakatole alifika katika Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Songwe na kueleza kuwa, Jerad Justine Kombe alimkopesha marehemu mume wake aitwaye Adam Mwakatole kiasi cha shilingi 15,000,000 mnamo tarehe 21.12.2016.

"Katika taarifa hiyo alieleza kuwa baada ya marehemu mume wake kufariki bwana Jerad Justine Kombe alibadilisha deni hilo na kulipandisha kuwa shilingi 40,000,000 au kuchukua nyumba ya marehemu iliyokuwa imewekwa rehani kama dhamana ya mkopo huo.

"Baada ya kupata taarifa ofisi yetu ilifanyia kazi taarifa hiyo. Ofisi yetu ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa mkopeshaji huyo bwana Jerad Justine Kombe hajasajiriwa kisheria kama kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha Sura ya 342 na Sheria ya Benki Kuu na Kanuni zake.

"Aidha uchunguzi ulibaini kuwa marehemu alipokuwa anakopa hakumshirikisha mke wa ndoa ili kupata idhini ya kuweka hati ya kiwanja kama dhamana ya mkopo kinyume na kifungu cha 59 cha sheria ya ndoa sura ya 29 mapitio ya mwaka 2019.

"Baada ya kujiridhisha kuwa mkopo huo ulikuwa umekiuka Sheria za nchi, ofisi ya TAKUKURU ilimtaka mama mjane Agness Adam Mwakatole kulipa kiasi cha shilingi 15,000,000 ambao ndio mkopo aliochukua marehemu mume wake badala ya shilingi 40,000,000 aliyokuwa akidaiwa au kutoa nyumba. Aidha ofisi yetu ilimtaka bwana Jerad Justine Kombe kukubali kupokea kiasi hicho na kumkabidhi hati ya kiwanja mama huyo,"amesema Mkuu huyo.

Amesema kuwa, wananchi wanapaswa kujiepusha na mikopo umiza. Pia wanapaswa kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano haya kwa ustawi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Taifa letu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news