KAMPUNI ya Mafuta ya Total Tanzania imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa kujenga mazingira wezeshi ya biashara na kuwawezesha Watanzania kupatiwa fursa za kuingia katika biashara ya vituo vya mafuta vya kiwango cha kimataifa, anaripoti MWANDISHI WETU.
Kituo hicho kipo kwenye moja ya barabara yenye shughuli nyingi za kiuchumi jijini Dar es salaam inayotokea Mbezi Beach hadi Mbezi Kimara hivyo kulenga kuwahudumia wakaazi wa Tegeta, Mbezi Beach na Kimara pamoja na watumiaji wote wa barabara hiyo.
“Napenda kutumia nafasi hii, kumshukuru Rais wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, na kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwezesha ukuaji wa kibiashara kwenye sekta ya nishati."Pia tunatambua kuwa uzinduzi huu usingewezekana pasingekuwa na baraka za Serikali ambayo waliidhinisha leseni za kuendesha kituo hiki na kwa hilo shukrani zangu za dhati zinaenda kwa EWURA pamoja na taasisi zingine za kiserikali zilizowezesha jambo hili kufanikiwa,”amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Total Tanzania,Jean Franchois Schoepp.
Jean Franchois ameongeza kuwa, Total Tanzania imekuwa ikihimiza wamiliki wa biashara kukuza biashara zao kwa kuingia ubia wa kibiashara na kampuni hiyo kwa njia ya DODO ambayo itawawezesha kumiliki na kuendesha vituo vya mafuta vyenye chapa ya Total.
DODO ni mfumo wa kibiashara ambao kampuni ya hiyo hutumia kuweza kuongeza mtandao wa vituo vyake nchini.
Mfumo huu unawawezesha wafanyabiashara kuingia kwenye ubia na Kampuni ya Total na kuweza kumiliki, kuendesha pamoja na kusimamia vituo vya huduma vya mafuta vyenye chapa ya Total.
Mkurugenzi Mtendaji wa Total Tanzania, Jean Franchois Schoepp amesema, Total inalenga kumfikia kila Mtanzania na kuwapatia nafasi ya kufuruhia huduma na bidhaa nzuri kutoka Total.
"Pia tunawaalika wafanyabiashara ambao wangependa kupanua biashara zao kuungana nasi kupitia mpango wetu wa DODO na kupata nafasi ya kumiliki kituo cha huduma ya mafuta na kuweza kupanua na kuimarisha biashara zao.
"Leo, tunafurahia kuingia katika ubia wa kibiashara na Mhandisi Frank Malle ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya F.S Mshuwa Co na mmiliki wa kituo hichi. Kwa ushirikiano huu tunatarajia kuihudumia Goba na jamii inayoishi maeneo ya jirani.
"Pia ningependa kutumia fursa hii kuwaalika wafanyabiashara ambao wangependa kupanua biashara zao kuungana nasi kupitia mpango wetu wa DODO na kupata nafasi ya kumiliki kituo cha huduma ya mafuta na kuweza kupanua na kuimarisha biashara zao,"amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Total Tanzania.
Kwa upande wake, mmiliki wa kituo hicho, Mhandisi Frank Malle ameishukuru Total sio tu kwa kuwawezesha kumiliki kituo hicho, bali pia kuwaokoa wasiuze ardhi yao, maana walishawishiwa sana kuuza ardhi, lakini Total ikawakomboa, sasa na wao ni wamiliki wa kituo cha kisasa cha mafuta cha Total.