TRA yawataka wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa kulipa kodi mapema, Mara yawakutanisha pamoja

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imewataka wafanyabiashara katika Manispaa ya Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla, kuendelea kuwa wazalendo kwa kulipa kodi kwa wakati na kuepukana na ukwepaji na ucheleweshaji ili kuiwezesha Serikali kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya Watanzania, anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini), Mara

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Elimu Mwandamizi Huduma kwa Mlipakodi Mkoa wa Mara, Zake Willbard wakati akitoa semina kwa wafanyabiashara wa Manispaa ya Musoma iliyofanyika katika Ukumbi wa Afrilux.

Wafanyabiashara katika Manispaa ya Musoma wakifuatilia mafunzo ya semina juu ya mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka 2020/2021, na namna ya kutuma ritani zao za kodi kwa njia ya mtandao. Semina hiyo imeendeshwa na Afisa Elimu Huduma kwa Mlipa Kodi Mkoa wa Mara, Zake Willbard katika Ukumbi wa Afrilux Musoma. (Diramakini).


Afisa huyo amewakumbusha wafanyabiashara hao wajibu wao wa kisheria wa kulipa kodi, kuwaelimisha juu ya mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi kwa mwaka 2020/2021 pamoja na namna ya kutuma ritani za kodi kwa njia ya mtandao.

Zake amesema kuwa, TRA Mkoa wa Mara inathamini kwa dhati mchango wa wafanyabiashara katika kuchangia maendeleo kupitia kodi wanazolipa serikalini na ndiyo maana imeendelea kushirikiana nao bega kwa bega kwa kila hatua ikiwemo kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati, kusudi waweze kufanya biashara katika mazingira bora na wezeshi,hatua ambayo itasaidia pia wao kulipa kodi za Serikali kwa wakati na kuepukana na adhabu kwa mujibu wa sheria.

"Kodi mnazolipa ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu, tumezidi kuendelea kuweka mazingira mazuri na mahusiano mema kila kukicha, lengo ni kuona kwamba mnapata faida nzuri katika biashara zenu ili na ninyi sasa muweze kulipa kodi ambazo ndiyo chanzo cha Serikali kujenga vituo vya afya, zahanati, miradi ya barabara na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi, niwaombe mzingatie kulipa kodi kwa wakati ili kuepukana na adhabu ambazo hutolewa,"amesema Zake.

Zake ameongeza kuwa,mamlaka hiyo Mkoa wa Mara imejipanga kuwafikia wafanyabiashara kila wilaya kuwapa elimu juu ya kodi, mabadiliko ya sheria ya kodi huku akisisitiza pia wafanyabiashara wazidi kuzingatia kutoa risti kwa wateja na wateja kuomba risti baada ya kununua bidhaa.

Jovina Mwita na Ghati Yusuph ambao ni wafanyabiashara katika Manispaa ya Musoma wameieleza Diramakini kuwa, wanaipongeza TRA Mkoa wa Mara kwa namna ambavyo imeimarisha mahusiano na wafanyabiashara.

Wamesema, hatua hiyo imekuwa ikishughulikia kwa wakati changamoto zao pindi wanapoziwasilisha jambo ambalo limeleta ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, na wameomba izidi kufika maeneo yote ya mkoa kutoa elimu.

Naye Katibu wa Chama cha Wafanyabiashara, Kilimo na Wenyevi viwanda (TCCIA) Mkoa wa Mara, Francis Ngowi akizungumza baada ya semina hiyo, amewashauri wafanyabiashara wote mkoani Mara kujiunga na chama hicho ili kuwa na sauti moja juu ya masuala mbalimbali katika kuimarisha biashara zao, ambapo wataweza pia kunufaika na fursa zilizopo TCCIA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news