TRA yawataka wafanyabiashara kuwa wakweli wanapotuma ritani za kodi kuepuka mikono ya sheria

Wafanyabiashara Wilaya ya Bunda na Mkoa wa Mkoa kwa ujumla wamesisitizwa kuwa wakweli na waaminifu katika kutuma ritani za kodi zao Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa njia ya mtandao,badala ya kutumia mwanya huo kutuma ritani za udanganyifu ili kulipa kodi ndogo isiyoendana na uhalisia wa biashara zao na mwisho zitaleta madhara kwenye biashara zao kwa kutozwa riba, adhabu na faini,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.

Afisa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi Mkoa wa Mara,Zake Willbard akiendesha semina kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Bunda kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka 2020/2021 pamoja na namna ya kutuma ritani TRA kwa mfumo wa mtandao. Semina hiyo imefanyika Ukumbi wa Land Masters Bunda. (Picha na Amos Lufungulo/Diramakini).

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Elimu Mwandamizi na Huduma kwa Mlipa Kodi Mkoa wa Mara, Zake Willbard wakati akitoa semina kwa wafanyabiashara ya mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi kwa mwaka 2020/2021 na namna ya kutuma ritani za kodi kwa njia ya mtandao kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Bunda iliyofanyika Ukumbi wa Land Masters.

Amesema kuwa, ukweli unahitajika sana kwa wafanyabiashara wote katika utumaji wa ritani zao, kwa kuweka viambatanisho vya kweli vyenye ushahidi panapohitajika kufanya hivyo, badala ya kufanya udanganyifu ama kutuma ritani sizizozingatia ukweli na kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na amesisitiza wazingatie ukweli ili kuepukana na mkono wa sheria.

Wafanyabiashara Wilaya ya Bunda wakifuatilia mafunzo ya semina ya mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka 2020/2021 iliyoendeshwa na Afisa Elimu Mwandamizi na Huduma kwa Mlipa Kodi Mkoa wa Mara, Zake Willbard iliyofanyika Land Masters Mjini Bunda.(Picha na Amos Lufungulo/Diramakini).

Zake amewasisitiza wafanyabiashara wilayani Bunda kuzingatia utoaji wa risti za kielektroniki (EFD) kwa asilimia 100 wanapouza bidhaa na wananchi wajijengee tabia ya kuomba risti wanaponunua bidhaa jambo ambalo Serikali imekuwa ikisisitiza wakati wote na lina manufaa kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.

Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka 2020/2021 Zake amesema, upande wa sheria ya vyombo vya moto imeanzisha kodi ya usajili kwa namba ya pekee ambapo shilingi 500,000 itaongezwa kwenye usajili, lengo ni kumuwezesha mteja kuwa na namba anayoipenda kwenye mfumo wa usajili na kuiwezesha Serikali kuongeza mapato.

Amesema, pia sheria ya Kodi ya Mapato kifungu cha 16 kimerekebishwa kwa kuongeza kifungu kidogo (1)( d)na (e) ili kutambua makato yatokayo kwenda kwenye uokoaji wa kodi ambapo kifungu (d) ni michango kwenye mfuko wa UKIMWI na (e) michango kwa ajili ya mapambano dhidi ya Corona lengo ni kuhamasisha uchangiaji wa hiari, lakini kifungu( e) kitasitishwa pale Waziri atakapotoa tamko la kusitisha uchangiaji huo.

Naye Meneja wa TRA Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara, Dickson Kamara amewaomba wafanyabiashara wilayani humo kufika ofisi za Mamlaka hiyo pindi wanapotatizwa kutuma ritani zao kwa mfumo wa mtandao kuepuka kukosea, huku akiwasisitiza waendelee kushirikiana kwa pamoja pale wanapotatizwa na changamoto mbalimbali kuzipatia ufumbuzi katika kufikia malengo chanya ya kukusanya kodi.

Nao wafanyabiashara wa Bunda, Paschal Yusuph na Neema Paul wameieleza Diramakini kuwa, wanaishukuru TRA Mkoa wa Mara kwa kuwafikia na kuwapa elimu juu ya mabadiliko ya sheria za kodi na namna ya kutuma ritani zao kwa mfumo wa mtandao, jambo ambalo litaongeza ufanisi katika shughuli zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news