Umoja wa vyama vya siasa nchini walaani vitendo visivyokubalika Pemba

Umoja wa Vyama vya Siasa Zanzibar umelaani vikali kitendo kilichotokea Pemba cha wananchi watatu kupigwa mapanga wakiwa msikitini, jambo ambalo wamesema hawaliungi mkono na wanalikemea kwa nguvu zote, kwani linaweza kuleta vurugu na kuondosha amani iliyoimarika nchini,anaripoti Mwandishi Diramakini.
(Diramakini)

Wamesema, kitendo hicho kilichotokea ni ishara ya uvunjifu wa amani, hivyo wameiomba Serikali ya Mapinduzi chini ya usimamizi wa Rais wa Zanzibar, Dkt.Ali Mohamed Shein kuchukua hatua za haraka kwa waliohusika ili iwe fundisho kwa wenye malengo ya kutenda uovu huo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vyama vya Upinzani,Ameir Hassan Ameir ambaye ni Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Demokrasia Makini ameyasema hayo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani uliopo Kikwajuni jijini Zanzibar.  Baadhi ya vyama ambavyo kwa pamoja vimelaani tukio hilo ni Chama cha SAU, DP, UPDP, DEMOKRASIA MAKINI ,TLP na UND.

Ameyasema hayo wakati walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na matendo hayo maovu, ambayo yaliyotokea juzi alfajiri huko kisiwani Pemba.

Wamesema,hali hiyo isifumbiwe macho, kwani amani ni kitu muhimu duniani na endapo itatoweka haitaweza kurudi tena na wanawake na watoto wataangamia mara moja hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi. 

Hamadi Mohamed Ibrahim ambaye ni Mgombea Urais Zanzibar kupitia Chama cha UPDP amesema, vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuchukua haraka ili kuhakikisha wote waliohusika na matendo hayo wanawajibika.

Wakati huo huo, kwa pamoja wamelaani kitendo cha kupigwa wananchi wenzao wakiwa ndani ya nyumba ya ibada na kusema hilo halitafumbiwa macho kwa kutaka vyombo vya ulinzi na usalama kulifanyia kazi mara moja na kuepuka umwagikaji wa damu usiendelee.

Kwa upande wake,Makamu Mwenyekiti wa Chama cha DP na Mgombea Ubunge Jimbo la Fuoni, Peter Agarton Mwagira amekemea uvunjifu wa amani akisema,kila wakati viongozi wa Serikali wanahimiza amani, "leo iweje waichezee".

“Kwa umoja wetu tunahakikisha tunayalinda Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na pia kulinda Muungano wetu uliodumu kwa miaka mingi,”vyama hivyo kupitia umoja huo vilitoa tamko na msisitizo wa pamoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news