MAMLAKA ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imewachukulia hatua wadaiwa sugu wa maji katika maeneo ya Tabata, Ubungo na Buguruni Mnyamani kwa kuwafikisha Mahakama ya Mwanzo Ilala jijini Dar es Salaam. Wadaiwa hao wanadaiwa bili za maji zaidi ya shilingi milioni 8,015,187.4.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Afisa Sheria kutoka DAWASA, Omary Kipingu imewataja washtakiwa waliofika leo kuwa ni, Ahad Gurisha mkazi wa Kisukuru Tabata ambaye anadaiwa shilingi 2,957,162, ambapo amepunguza shilingi 400,000, Tune Juma mkazi wa Kibangu, Ubungo ambaye anadaiwa shilingi 584,707.15,
Washtakiwa wengine ambao hawajafika leo licha ya mahakama kutoa hati ya wito wa kuitwa mahakamani ni, David Mgaya kutoka Tabata ambaye anadaiwa shilingi 1,085,178.15, Rahima Sarakikya mkazi wa Buguruni anadaiwa shilingi 747,852.45, Hassan Khamis mkazi wa Buguruni Mnyamani anadaiwa shilingi 733,008.45, Zacharia Okoth mkazi wa Tabata anadaiwa shilingi 592,964.35 na Ashura Embe Mkazi wa Buguruni Mnyamani ambaye anadaiwa shilingi 1,314,314.85.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka mbele ya mahakimu wawili tofauti ambapo, Gurisha na Juma wamesomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Nahato na walikubali kuwa ni kweli wanadaiwa na mamlaka hiyo.
Naye Juma aliyeingia makubaliano ya kulipa deni hilo ni mama mwenye nyumba wake, Gregory Kahwili ambae aliahidi kuwa Septemba 30,2020 atalipa 200,000, ambapo deni lililobaki atalipa kila mwezi 100,000 litakamilika Januari 30,2021.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imetoa agizo la mwisho kwa wadaiwa hao kufika mahakamani hapo, ambapo imetoa hati ya wito kwa wadaiwa hao ambao watatakiwa kufika mahakamani hapo, Septemba 11, mwaka huu.