Ushauri huo, aliutoa mara baada ya kutembelea Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Wakati huo huo, Waziri Biteko ametoa pongezi kwa waandaji wa maonesho hayo ambayo mwaka huu zaidi ya kampuni 420 zinashiriki.
Vilevile, Waziri Biteko ametoa wito kwa taasisi za kibenki kuendelea kuwalea wachimbaji wadogo na wafanyabiashara ya madini kwa kuwapa mafunzo pamoja na mikopo ili wazalishe kwa faida.
Naye Mkurugenzi wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo wa NBC, Elibariki Masuke alisema,benki hiyo mkoani hapa imetoa mkopo wa zaidi ya shilingi bilioni 4.4 kwa wadau wa Sekta ya Madini mkoani humo ili kuwaongezea uwezo katika shughuli zao.
Hayo aliyasema mbele ya Waziri Biteko alipotembelea banda la la benki hiyo katika Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Imeelezwa kuwa, wanufaika wa mikopo hiyo ni pamoja na wachimbaji wadogo,wafanyabiashara ya madini na wachenjuaji wa madini wa Mkoa wa Geita.
"Sisi kama Benki ya NBC tumeanza kutoa mafunzo kwa wadau wa madini hususan wachimbaji wadogo wa dhahabu na wafanyabiashara ya dhahabu ili kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuwekeza katika Sekta ya Madini,"alisema Masuke.
Pamoja na mambo mengine, Masuke alisema Benki ya NBC imekuwa mdau mkubwa kwenye Sekta ya Madini ambapo mpaka sasa kuna taratibu zinawekwa sawa ili mikopo mikubwa zaidi ianze kutolewa kwa wadau wa Sekta ya Madini kote nchini.