OFISI ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maendeleo ya Uwekezaji imekutana na wadau wa uwekezaji wa sekta ya umma kwa lengo la kuidhinisha taarifa ya tathmini ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996.
Wadau hao ni kutoka Wizara, Idara, Taasisi na Wakala wa Serikali. Baada ya kupokea taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa sera hiyo, wameridhishwa kwa jinsi ilivyobainisha nchi inavyoweza kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje.
Wakipongeza wakati wa kujadili taarifa hiyo, Septemba 11, 2020 jijini Dodoma. Wadau hao wamesisitiza tathmini hiyo iliyojikita kwenye masuala ya kisera, kisheria na kiutendaji inaendelea kutoa mapendekezo ya kuendelea kutatua changamoto za uwekezaji nchini hususani kwenye maeneo ya Uratibu wa Masuala ya Uwekezaji, Utangazaji wa Fursa za Uwekezaji, Uwezeshaji Uwekezaji, pamoja na Vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko akifungua warsha ya wadau wa uwekezaji sekta ya umma iliyolenga kuidhinisha taarifa ya tathmini ya sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 Septemba 11, 2020 jijini Dodoma, kikao kazi hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Akiongea wakati akifungua kikao kazi hicho, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Bibi Dorothy Mwaluko amesisitiza kuwa upo umuhimu wa wadau hao kubainisha masuala ya kisera, kiutendaji na kisheria, ili kuhakikisha kuwa Sera ya Taifa ya uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji nchini haikinzani na sheria nyingine za kisekta kwenye masuala ya uwekezaji.
“Serikali imekuwa ikitunga Sera na Sheria kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara nchini, tunahitaji kuwa na Sera madhubuti za kuvutia na kuwezesha uwekezaji katika sekta zote ili kutumia vilivyo fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini,"amesisitiza Mwaluko.
Sera ya Taifa ya Uwekezaji imebainisha malengo mahsusi sita (6) na malengo nane (8) ya kisekta. Baadhi ya malengo hayo ni kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa kwa ajili ya mauzo ya nje; Kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi; Kuhimiza na kuvutia matumizi ya teknolojia za kisasa katika uwekezaji; Kuweka mfumo mzuri na wa wazi wa kisheria; na kuondoa urasimu katika taratibu za upatikanaji wa vibali vya uwekezaji.
Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 na Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1997 iliyoanzisha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), vinaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara za kisekta, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Idara, Taasisi na Wakala wa Serikali. Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimepewa jukumu la kuratibu, kuvutia, kutangaza na kuwezesha wawekezaji hapa nchini.