JESHI la Polisi mkoani Njombe linawashikiliwa vijana wawili wanaojulikana kwa majina ya Masoud Mang’ombe na Hamis Ismael kwa tuhuma za kuvunja ofisi ya Mahakama ya Wilaya ya Njombe na kuiba kopyuta mpakato tatu, mashine moja ya POS na kilo 25 za sukari.Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issa amesema tukio la kuvunja Mahakama na kuiba vitendea kazi na sukari lilitekelezwa Julai 15,mwaka huu na watuhumiwa kukamatwa Septemba 4, mwaka huu.
Pia jeshi hilo limebainisha kuwa,siku za hivi karibuni kumeibuka wimbi la wizi wa vipuri vya magari ambapo katika jitihada za kudhibiti uhalifu huo watuhumiwa sita ambao wanatajwa kuwa kwenye mtandao huo wa wizi wamekamatwa.
Kamanda huyo amesema, jeshi hilo limejipanga vema na kila ambaye anadhamiria kufanya vitendo vya uhalifu atambue kuwa mipango yake haitafanikiwa huku akiendelea kuwahamasisha wananchi kuendelea kutoa taarifa juu ya matendo yoyote ambayo yanaviashia vya kihalifu.